Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema uzinduzi wa shamrashamra kuelekea kileleni cha wiki ya Mwananchi utafanyika August 04 wilaya ya Katoro mkoani Geita.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari mapema leo, Kamwe alisema maandalizi kuelekea tukio hilo yamekamilika ambapo wenyeji wao wametenga zaidi ya Tsh Milioni 147 kwa ajili ya tukio hilo kubwa ambalo litaambatana na burudani na pamoja na kuendeleza utamaduni wa Wananchi kunywa supu ng'ombe wa kutosha wakiandaliwa kwa ajili ya tukio hilo pamoja na nyama choma.
Kamwe alitangaza rasmi kilele cha wiki ya Mwananchi ni August 09 uwanja wa Uhuru ambapo Mwenyekiti huyo wa wasemaje akatangaza viingilio vya Tamasha hilo ambalo linafanyika uwanja wa Uhuru kwa mara ya kwanza baada ya uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa kutokana na ukarabati unaoendelea.
Viingilio;
- Royal - Tsh 300,000/- pamoja na jezi mpya ya msimu iliyosainiwa na mchezaji umpendae, usafiri wa kwenda na kurudi uwanja wa Uhuru kutoka Serena, viburudisho
- Vip - Tsh 100,000/-
- Mzunguuko - 20,000/-
Kamwe amewataka mashabiki na wanachama wa Yanga kuchangamikia tiketi zao mapema kwani uwanja wa Uhuru ni mdogo kulinganisha dimba la Mkapa ambapo kuna tiketi 19,000 tu za Mzunguuko.
Aidha timu ambayo itachuana na Yanga kwenye Tamasha hilo itatangazwa baada ya Mkutano Mkuu wa mwaka unaombatana na uchaguzi utakaofanyika August 02.
“Baada ya mkutano mkuu wa Yanga Sc utakaofanyika Siku ya tarehe 02 tutawatangazia timu ambayo tutakwenda kucheza nayo siku ya Mwananchi”
“Tamasha la Wiki ya Mwananchi la msimu huu limeongezeka thamani kwa sajili tulizofanya maana mashabiki kwa mara ya kwanza watapata nafasi ya kuwashuhudia wachezaji wetu wakiwa wanacheza klabu ya Yanga sc kwenye uwanja wa uhuru siku ya tarehe 09,” alisema Kamwe