Namba 6 ya Yanga bado inatamba huko kwenye mitandao ya kijamii Wananchi wakisubiri kumfahamu mchezaji huyo mwenye 'profile' kubwa ambaye Yanga imemsajili kuimarisha eneo la kiungo mkabaji.
Ni ukweli usiofichika tangu kuondoka kwa Khalid Aucho, Yanga haijapata mbadala wake, wakati huu Injinia Hersi Said amefanya kazi kubwa kwenye dirisha la usajili kuhakikisha mchezaji sahihi katika eneo hilo anapatikana.
Tetesi zimekuwa nyingi, lakini sasa ni wazi muda si mrefu kitendawili cha namba 6 kinakwenda kuteguliwa.
Kiungo wa Olympic Club de Safi ya Morocco Fred Ngoma ameibuka kwenye tetesi za karibuni kuwa huenda akatua kwa Wananchi.
Vyanzo vya karibuni na mchezaji huyo kutoka Congo Brazaville, vimethibitisha kuwa mazungumzo yamefanyika, makubaliano kufikiwa na kuna uwezekano mkubwa nyota huyo akawa miongoni mwa wachezaji wawili wa kigeni wanaokwenda kufunga usajili wa kimataifa wa Yanga.
Ngoma ni nani?
Ngoma ni kiungo mwenye umri wa miaka 28 raia wa Congo-Brazzaville, msimu uliopita aliitumikia Olympique Club de Safi (OC Safi) inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro). Alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichocheza nusu fainali ya kombe la Shirikisho (CAFCC).
Uzoefu na wasifu wake
Ngoma, aliyezaliwa Novemba 24, 1997 huko Pointe-Noire, ana wasifu mkubwa na uzoefu wa kutosha katika soka la Afrika. Alianzia soka la ushindani nchini mwao akizichezea klabu za CSMD Diables Noirs, AC Léopards, na CS La Mancha, kabla ya kung'ara zaidi na AS Otôho kati ya mwaka 2018 na 2021. Akiwa na Otôho, alicheza michuano ya kimataifa ya CAF na kuitwa Timu ya Taifa ya Congo-Brazzaville.
Mbali na nyumbani kwao, kiungo huyo ana uzoefu wa miaka mingi katika soka la Kaskazini mwa Afrika. Alicheza nchini Tunisia akiwa na CA Bizertin (2021–2023), kisha akatimkia Libya kuziwakilisha Al-Ittihad Tripoli na Al-Akhdar.
Katika msimu uliopita nchini Morocco akiwa na OC Safi, Ngoma alikuwa nguzo muhimu ambapo alicheza jumla ya michezo 27 ya Ligi Kuu (Botola Pro) na kukusanya dakika 2,138.
Kuziba Pengo la Namba 6
Usajili wa Ngoma unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Yanga kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mkabaji (Namba 6).
Mchezaji huyo mwenye urefu wa mita 1.73 anasifika kwa mtindo wake wa uchezaji wa nguvu, kukata pasi za wapinzani, na uwezo wa kucheza pia kama beki wa kati au kiungo wa kati (Box-to-Box).
Ni wazi usajili wa mchezaji huyu unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika kikosi cha Yanga kuelekea michuano ya kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).
Ngoma alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na OC Safi lakini baada ya timu hiyo kushuka daraja ligi kuu ya Morocco, gharama ya kuvunja mkataba wake imepungua kwa zaidi ya asilimia 50 na kufikia takribani Mil 600.
Katika mkataba huo kulikuwa na kipengele cha kumruhusu aondoke kwa gharama hiyo endapo OC Safi itashuka daraja.