Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said jana alitambulisha usajii wa kiungo mkabaji Fred Ngoma, huku tukio hilo likivunja rekodi kwa kuvutia mamilioni ya watazamaji kupitia majukwaa mbalimbali.
Ngoma, raia wa Congo-Brazzaville, amesajiliwa kutoka klabu ya Olympique Club de Safi (OC Safi) ya Morocco kwa ajili ya kuongeza nguvu katika eneo la kiungo cha ukabaji, ambalo limekuwa likihitaji maboresho tangu kuondoka kwa Khalid Aucho.
Utambulisho wa kiungo huyo umeingia katika historia ya soka la Afrika Mashariki baada ya kufuatiliwa na mashabiki wengi kupitia televisheni na majukwaa ya kidijitali. Azam Sports 1 ilifikia watazamaji milioni 12, huku Instagram Live ikivuta watazamaji 71,550 na YouTube Live ikifikia 69,000.
Idadi hiyo ya watazamaji imeufanya utambulisho wa Ngoma kuwa moja ya matukio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika usajili wa wachezaji Afrika Mashariki, ikiashiria kuongezeka kwa ushawishi wa soka la ukanda huo kwenye majukwaa ya kidijitali.

