Mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga dhidi ya Simba SC leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkalihuku historia ya mashindano haya ikiipa Yanga nafasi ya kujivunia rekodi yake.
Ngao ya Jamii ilianzishwa rasmi mwaka 2001, ambapo mchezo wa kwanza uliwakutanisha Yanga na Simba. Yanga iliweka historia kwa kutwaa Ngao hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi.
Kuanzia mwaka 2002 hadi 2008, hakukuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii baada ya mashindano hayo kusitishwa. Yakarejea tena mwaka 2009 na kuendelea mpaka sasa.
Kwa jumla ya historia ya mashindano hayo, Yanga SC ndiyo inayoongoza kwa kutwaa Ngao ya Jamii mara nyingi zaidi, ikiwa imefanikiwa kubeba taji hilo mara 9. Inafuatwa na Simba SC, ambayo imelitwaa mara 7. Azam FC na Mtibwa Sugar kila moja imetwaa Ngao ya Jamii mara moja.
Katika miaka ya hivi karibuni, Yanga imeendelea kuonyesha ubabe mkubwa katika mashindano haya, ikitwaa Ngao mwaka 2021, 2022, 2024 na 2025. Simba, kwa upande wake, ilitwaa taji hilo mara nne mfululizo kuanzia 2017 hadi 2020, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa uliopo kati ya vigogo hao wa soka la Tanzania.
Hivyo, mchezo wa leo unaongeza sura nyingine katika historia ndefu ya Ngao ya Jamii na pia katika ushindani wa jadi kati ya Yanga na Simba. Yanga itakuwa ikilenga kuendeleza ubabe wake na kuongeza idadi ya mataji, wakati Simba itatafuta ushindi utakaoiwezesha kurejesha Ngao hiyo upande wa Msimbazi.
Dakika 90 za mchezo baina ya timu hizo zitaamua mshindi pale uwanja wa New Amaan Complex, saa 2:30 usiku. Endapo hakutakuwa na mshindi baada ya dakika 90, mikwaju ya penati itaamua