Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, alionyesha ubora wake wa kiufundi katika mchezo dhidi ya Simba baada ya kufanikiwa kuzima moja ya silaha kubwa za wapinzani wao, mashambulizi kupitia pembeni.
Silaha kubwa ya Simba katika kutengeneza mashambulizi ni winga wake wawili, Libasse Gueye na Anicet Oura. Wawili hao wamekuwa tegemeo kubwa la Simba katika kuvuruga safu za ulinzi kwa kutumia kasi, uwezo wa kupiga krosi na kuingia ndani kutoka pembeni. Lakini safari hii Manqoba alikuwa amejiandaa.
Kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns alifahamu mapema kwamba iwapo angewaacha Gueye na Oura wapate nafasi ya kucheza kwa uhuru, Simba ingeweza kupata faida kubwa. Ndiyo maana aliweka mkakati maalum wa kuwadhibiti kwa kuwatumia Yao Kouassi na Chadrack Boka.
Yao alipewa jukumu la kuhakikisha upande wake unakuwa salama, huku Boka akifanya kazi hiyo upande wa pili. Wachezaji hao wawili walipata msaada mkubwa kutoka kwa viungo wa kati Maxi Nzengeli, Duke Abuya na Mudathir Yahya, ambao walikuwa wakibadilishana nafasi na kusaidia kuziba mianya iliyokuwa ikitokea pembeni.
Yao Kouassi alikuwa kila mahali
Pengine kama kungekuwa na tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo, jina la Yao Kouassi lingekuwa miongoni mwa yanayostahili kupewa tuzo hiyo.
Yao hakuwa na kazi ya kuzuia tu. Alionekana kuwa na mchango mkubwa katika maeneo yote mawili, ulinzi na ushambuliaji.
Uwezo wake wa kupanda mbele na kurejea haraka kwenye nafasi yake uliifanya Simba kushindwa kutumia vizuri eneo hilo. Alifanyiwa madhambi mara nyingi kutokana na namna alivyokuwa akicheza na kutafuta nafasi, jambo lililoonyesha jinsi alivyokuwa kikwazo kwa wapinzani wake.

Boka alimfunga Libasse
Upande wa kushoto, Chadrack Boka alikuwa na kazi maalum ya kumzuia Libasse Gueye. Na kazi hiyo aliitekeleza kwa ufanisi mkubwa.
Libasse, ambaye mara nyingi amekuwa tishio kubwa kwa Simba kutokana na kasi na uwezo wake wa kucheza pembeni, safari hii hakupata nafasi ya kuisogelea kwa urahisi lango la Yanga. Boka alimdhibiti kwa karibu na kuhakikisha hakuna madhara makubwa yaliyotokea kupitia upande huo.
Utendaji huo unaonyesha kwa nini uongozi wa Yanga ulifanya uamuzi sahihi wa kuendelea kumbakisha Boka kikosini baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Katika mchezo huo alidhihirisha thamani yake na kama ataendelea kuwa fiti bila kusumbuliwa na majeraha, anaweza kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Yanga msimu huu.
Mbali na kazi yake ya ulinzi, Boka alionekana kuboresha zaidi upande wa kushambulia, hasa katika upigaji wa krosi.
Mchezo dhidi ya Simba ulitoa ushahidi wa hilo baada ya Boka kutengeneza bao pekee la mchezo lililofungwa na Albert Kangwanda dakika ya 31.
Kwa ujumla, Manqoba Mngqithi alionekana kuisoma Simba vizuri. Alijua silaha yake kubwa iko wapi na akaweka mpango wa kuifunga mapema.