Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, klabu ya Yanga SC, leo Jumamosi, Agosti 15, 2026, wanatarajiwa kuandika historia nyingine kwa kumtambulisha rasmi mchezaji wao mpya "X-Factor", katika Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es salaam.
Tukio hilo la kukata na shoka linatarajiwa kuanza rasmi saa 10:00 jioni, ambapo mashabiki na wanachama wa klabu hiyo watapata nafasi ya kushuhudia usajili unaotajwa kuwa wa kufunga hesabu za dirisha hili kibabe.
Klabu imetangaza kiingilio cha Shilingi 2,000 tu kwa jukwaa la kawaida, huku wamiliki wa kadi za kidijitali za ‘Black Card’ wakiandaliwa eneo maalum la VIP.
Uongozi wa Yanga umekuwa ukiweka jina la mchezaji huyo siri, ukitaka kuwapa sapraizi mashabiki wake.
Hata hivyo, taarifa za ndani kabisa kutoka Jangwani zinasema kuwa mchezaji huyo anaweza kuwa kiungo fundi wa mpira, Stephane Aziz Ki, ambaye anarejea klabuni hapo kwa mkataba mnono unaokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola za Kimarekani 800,000 (takribani Shilingi Bilioni 2 za Kitanzania), huku ufadhili mkubwa ukitoka kwa mdhamini wao mkuu, GSM.
KMC Complex sasa kuwa 'Chinjio' jipya la Yanga
Mbali na utambulisho huo, Yanga inatumia tukio la leo kuuzindua rasmi uwanja wa KMC Complex kama uwanja wao mpya wa nyumbani kwa mechi za ndani msimu huu wa 2026/2027.
Uamuzi huo unakuja baada ya klabu hiyo kuachana na mpango wa kutumia Uwanja wa Uhuru uliopo Temeke.
Burudani mbili ndani ya uwanja mmoja
Baada ya shamrashamra za utambulisho huo wa "X-Factor" kumalizika uwanjani hapo Mwenge, uongozi wa Yanga umeweka skrini kubwa ambapo mashabiki wote waliofurika KMC Complex watakaa pamoja kutazama mechi yao ya kwanza ya ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC, inayopigwa leo katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.