Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, wameanza msimu huu kwa ubabe wakiweka rekodi ya kutopoteza mchezo wa ufunguzi kwa msimu wa saba mfululizo, kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC.
Mchezo huo uliopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Majaliwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, ulishuhudia Yanga ikionyesha kiwango cha juu na kuwapa mashabiki wao matumaini makubwa ya katika mkakati wa kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa sita mfululizo.
Mara ya mwisho kwa miamba hiyo ya Jangwani kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ilikuwa ni msimu wa 2019/20, walipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting, lililowekwa wavuni na Sadat Mohamed.
Tangu hapo, Yanga imekuwa na mwendo wa kuwasha moto katika mechi zake za kwanza.
Beki raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Shadrack Boka, ameingia kwenye vitabu vya kumbukumbu vya klabu hiyo baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga msimu huu.
Boka alipachika bao hilo kwa kichwa akimalizia mpira wa kona.Bao hilo linafanya kuwa msimu wa pili mfululizo kwa Yanga kufungua msimu kwa mabao ya vichwa yanayotokana na kona.
Msimu uliopita, kiungo mshambuliaji Lassine Kouma, mwenye uraia pacha wa Mali na Chad, alifanya hivyo dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika ushindi wa mabao 3-0.
Kipigo hicho pia kimeongeza rekodi ya wachezaji wa kigeni kufunga mabao ya ufunguzi wa msimu kwa miaka mitatu mfululizo.
Katika msimu wa 2024/25, Maxi Nzengeli (raia wa DRC) ndiye aliyefungua akaunti ya mabao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Mzawa wa mwisho kufanya hivyo alikuwa Dickson Job katika msimu wa 2023/24, Yanga ilipoishindilia KMC mabao 5-0.
Aidha Nzengeli ameweka rekodi ya kufunga bao katika mechi ya kwanza ya msimu kwa misimu mitatu mfululizo.
Baada ya kukamilika kwa mchezo huo wa kwanza, Yanga sasa inaelekeza nguvu zake kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Alhamisi, August 20 kwenye uwanja wa KMC Complex