Uongozi wa Yanga SC umeweka wazi msimamo wake kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya klabu hiyo na beki wake wa kulia, Israel Patrick Mwenda, huku ukifichua mawasiliano rasmi yaliyofanyika baina ya pande hizo.
Akizungumza na Crown FM Radio, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, alisema klabu hiyo ina nyaraka zinazoonyesha hatua mbalimbali ilizochukua tangu mchezaji huyo kuondoka kambini bila kutoa taarifa kwa uongozi.
Mwenda aliomba mapumziko
Kwa mujibu wa Kamwe, Mwenda mwenyewe ndiye aliyeomba kupewa ruhusa ya kupumzika baada ya kueleza kuwa hakuwa katika hali nzuri ya kisaikolojia iliyomuwezesha kutekeleza majukumu yake ya soka kwa ufanisi.
Kamwe alisema mchezaji huyo aliwasilisha barua hiyo Julai 3, baada ya uongozi wa Yanga kumwandikia mara kadhaa ukimtaka kutoa maelezo kuhusu sababu za kuondoka kambini bila taarifa.
Uongozi wa klabu hiyo umesisitiza kuwa una ushahidi wa maandishi wa mawasiliano yaliyofanyika na Mwenda, ikiwa ni pamoja na barua na maelekezo yaliyotolewa kuhusu suala hilo.
Kutokuwepo kwa Mwenda kambini kulimfanya akose baadhi ya mechi muhimu zilizokuwa zikihitimisha msimu uliopita, jambo ambalo limeongeza mjadala kuhusu mustakabali wa beki huyo ndani ya klabu.
Yanga yajibu madai ya baba wa Mwenda
Ufafanuzi wa Yanga umefuatia pia kauli za baba mzazi wa mchezaji huyo, Mzee Patrick Mwenda, ambaye alizungumzia masuala yanayohusu maslahi ya mwanawe pamoja na madai ya kuzuiliwa kwa mishahara yake.
Hata hivyo, Kamwe alisema Yanga haishughulikii suala hilo kwa kusikiliza maoni ya kila mtu, bali inashughulikia kwa kuzingatia wahusika wanaotambuliwa kisheria ndani ya mkataba wa mchezaji, ambao unaelezwa kuwa unaendelea hadi mwaka 2028.
Mwenda atakiwa kuripoti
Katika hatua nyingine, Kamwe alisema Yanga imemwandikia Mwenda barua ya kumtaka aripoti na kufika mbele ya uongozi wa klabu ili kutoa maelezo kuhusu kutokuwepo kwake na kushiriki katika jitihada za kutatua mgogoro huo.
Kwa mujibu wa klabu, hatua hiyo inalenga kumpa mchezaji nafasi ya kueleza upande wake na kuweka wazi sababu zilizosababisha kutokuwepo kambini, badala ya suala hilo kuendelea kupotoshwa.