Beki wa kushoto wa Yanga, Chadrack Boka, ameanza msimu kwa kasi kubwa huku akionyesha kiwango kinachomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Kocha Manqoba Mngqithi.
Mkongomani huyo ambaye msimu uliopita alionekana kuwa kwenye hatihati ya kuendelea na safari yake ndani ya Yanga, sasa ameanza kutoa majibu uwanjani baada ya kuaminiwa na benchi jipya la ufundi.
Katika mechi tatu alizoanza msimu huu, Boka tayari ameweka mchango wake kwenye mabao ya Yanga akitoa asisti au kufunga kwenye kila mchezo aliocheza.
Alitoa asisti kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, akafunga kwenye mchezo dhidi ya Namungo Fc na kisha akatoa tena asisti kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union.
Kocha Manqoba ameeleza kufurahishwa na kazi inayofanywa na Mcongomani huyo ambaye ni kama amejimilikisha nafasi ya beki wa kushoto huku akisaidiana na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' ambaye Manqoba amemtumia kama winga kwenye baadhi ya mechi.
"Anaonyesha uwezo mkubwa wa kusaidia timu inaposhambulia, lakini pia anafanya vizuri kwenye majukumu ya ulinzi mara Yanga inapopoteza mpira," alisema Manqoba
Kocha huyo ameonyesha kuvutiwa zaidi na kasi, nguvu pamoja na matumizi mazuri ya kimo cha Boka, vitu ambavyo vimekuwa vikimsaidia katika ushindani wa mipira na kurejea kwa haraka kwenye eneo lake.