Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, amefurahia kurejea kwake kikosini na kuanza upya majukumu yake ndani ya klabu hiyo kwa kiwango kizuri, akiamini kuwa ari, kujituma na moyo wa kupambana wa wachezaji ndiyo siri ya kuendelea kwa ubabe wao msimu huu.
Yanga jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Ulikuwa mchezo maalum kwa Aziz Ki kwani ulikuwa mchezo wake wa kwanza kuichezea Yanga tangu arejeshwe kwenye usajili wa dirisha lililopita, akitokea klabu ya Al Ittihad ya Libya.
Aanzia pale alipoishia
Licha ya kuwa ulikuwa mchezo wake wa kwanza baada ya kurejea, Aziz Ki hakuhitaji muda mrefu kuonyesha alichonacho. Mchezaji huyo aliendelea pale alipoishia mara ya mwisho ndani ya kikosi cha Yanga kwa kutoa asisti ya bao la kwanza lililofungwa na Peter Shalulile dakika ya 26.
Uwepo wa Aziz Ki uliongeza ubora katika eneo la ushambuliaji la Yanga, huku kiungo huyo akionyesha utayari wa kupambana na kusaidia timu yake kupata matokeo.
Katika kipindi cha pili, Aziz Ki alikuwa karibu zaidi kuandika jina lake kwenye orodha ya wafungaji baada ya kupiga shuti kali akiwa nje kidogo ya eneo la penalti, lakini mpira huo uligonga mwamba na kurejea uwanjani.
Ajivunia kurejea Yanga
Baada ya mchezo huo, Aziz Ki ameonyesha furaha yake kwa kurejea kuichezea Yanga na kupata ushindi katika mechi yake ya kwanza.
Kiungo huyo ameeleza kujivunia kuwa sehemu ya kikosi hicho na kuwataka wachezaji wenzake pamoja na mashabiki wa Yanga kuendelea na mapambano ili kufikia mafanikio makubwa zaidi msimu huu.
“Kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kujitoa huleta matokeo mazuri mwishoni. Ninajivunia timu hii na ushindi huu. Tuendelee kusonga mbele. Mwananchi siku moja, Mwananchi daima,” aliandika Aziz Ki kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii
Ujumbe huo wa Aziz Ki unaonyesha wazi kuwa mchezaji huyo amerudi Yanga akiwa na kiu kubwa ya mafanikio na yuko tayari kuendelea kupambana na wachezaji wenzake kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo yake msimu huu.

