Yanga imetinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gaborone United katika mchezo uliopigwa uwanja wa Azam Complex.
Haukuwa mchezo mwepesi kwani Wananchi walilazimika kusubiri filimbi ya mwisho kushangilia ushindi kutokana na ushindani mkubwa dakika za lala salama.
Peter Shalulile alitangulia kufunga dakika ya 7 akimalizia pasi kutoka kwa Selemani Mwalimu aliyetengewa na Stephane Aziz Ki.
Yanga ilitawala mchezo kwa muda mwingi na pengiine walistahili kwenda mapumziko na zaidi ya bao moja Mwalimu akikosa nafasi adimu.
Kipindi cha pili Gaborone walizinduka wakisaka bao la kusawazisha huku Yanga ikiendelea kutengeneza nafasi zaidi lakini kikwazo kikawa mlinda lango wa Gaborone United.
Ni kama baada ya Aziz Ki na Peter Shalulile kutoka nafasi zao zikichukuliwa na Hussein Zakouane na Albert Kangwanda huku Mwalimu akisimama mbele peke yake kuliwapa ahueni Gaborone ambao walikuwa juu zaidi wakitawala mchezo.

Hata hivyo ilikuwa na Yanga iliyofunga bao la pili dakika ya 83 kupitia Cheick Ibrahim Toure aliyeingia kuchukua nafasi ya Mwalimu akimalizia kazi nzuri ya Kangwanda.
Gaborone walifunga bao la kufutia machozi kwenye dakika ya 86 na unaweza kusema kuingia kwa bao hilo kuliiongezea Yanga presha dakika za lala salama lakini mwisho wa siku Yanga iliweza kuibuka na ushindi huo uliowafanya washinde kwa mabao 3-2 na kufuzu raundi ya kwanza.