Jana Yanga ilifanikiwa kufuzu raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa kwa ushindi wa jasho jingi wa mabao 2-1 mbele ya Gaborone United ya Botswana.
Jambo muhimu kwa Yanga ni kufuzu hatua inayofuata lakini ni wazi haikuwa rahisi mbele ya vijana wa Sean Connor.
Ulikuwa mchezo wa vipindi viwili, Yanga ikitawala kipindi cha kwanza huku wapinzani wao wakija juu kwenye kipindi cha pili.
Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi kubwa na kuwaduwaza wapinzani wao ambao dakika 20 za kwanza walijikuta wakibaki nyuma kwa muda mwingi huku Yanga ikitumia utawala wake kufunga bao la mapema kupitia Peter Shalulile.
Kulikuwa na nafasi nyingine ikiwemo ya Selemani Mwalimu ambayo kama angeitumia vyema pengine Yanga ingemaliza mechi hiyo kwenye dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Baada ya mapumziko Gaborone United waliongeza presha kusaka bao la kusawazisha, tayari walikuwa nyuma kwa bao 1-0 na hivyo hawakuwa na cha kupoteza.
Walichukua 'risk' na kusogea wengi mbele na hapo ndipo presha ilianza kuonekana upande wa Yanga. Wapo wanaomlaumu kocha Manqoba Mngqithi kwa mabadiliko aliyofanya kwa kuwatoa Peter Shalulile na Stephane Aziz Ki, lakini ni wazi mpango wake ilikuwa kutumia kasi ya wachezaji walioingia Albrert Kangwanda na Hussein Zokouane kuwashitukiza Gaborone United ambao walikuwa wakiacha mianya mingi nyuma.
Mpango huo ulifanikiwa kwani bao la pili la Cheick Ibrahim Toure lilitokana na shambulizi la kujibu Kangwanda akimtengenezea Toure kufunga bao la pili.
Hata hivyo kupotea kwa umakini kwa nahodha Bakari Mwamnyeto akapoteza mpira wakati timu inajenga mashambulizi, Gaborone wakatumia mwanya huo kutengeneza shambulizi ambalo liliwapatia bao dakika ya 86.
Kuingia kwa bao hilo kuliongeza presha zaidi ya mchezo kwani kama Gaborone wangefunga bao jingine Yanga ingeondoshwa mashindanoni.
Akizungumza baada ya mchezo kocha mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi alisema alikuwa na mpango mzuri kwenye kipindi cha pili lakini utekelezaji wake haukufanyika kama alivyotarajia lakini jambo muhimu kwake ni ushindi huo uliowapeleka raundi ya kwanza.
"Ni mechi ambayo ilikuwa mikononi mwetu kwa muda mwingi, hatukutumia nafasi zetu kumaliza mchezo mapema. Ndivyo ilivyo kama hutumii nafasi unajiongezea presha, hii ni mechi ambayo tungeweza kushinda kwa mabao mengi lakini nafurahi, wachezaji wamepambana na tumefanikiwa kupata ushindi tuliohitaji na kusonga mbele hatua inayofuata," alisema Manqoba.
Gaborone walionekana kuwa na dhamira ya kufanya jambo kwenye hatua hii kwani walijipanga ndani na nje ya uwanja.
Kuna matukio mengi yalijiri kabla ya mchezo huo, Gaborone walionekana kufanya matukio yanayohusiana na masuala ya kishirikina bila ya woga.
Walifanya hivyo kwenye mchezo wa kwanza kwao na wakarudia tena uwanja wa Azam Complex siku walipofanya mazoezi ya mwisho na hata jana kabla ya mchezo.
Pia Gaborone imeonekana kuwa timu imara kiufundi, wanaweza kucheza aina zote za soka. Mechi iliyopita walipaki basi lakini jana wakaamua kufunguka hasa kwenye kipindi cha pili na kuipa Yanga changamoto.
Ama kwa hakika ilikuwa mechi yenye hadhi ya hatua ya makundi ambayo kwa bahati mbaya imechezwa hatua ya awali.