Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi ameonyesha imani kubwa na kikosi chake akienda mbali kwa kutamka kuwa anayo timu ya kutwaa taji la ligi ya mabingwa barani Afrika.
Juzi Yanga ilivuka hatua ya awali ya michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya Gaborone United baada ya ushindi wa mechi ya marudiano dimba la Azam Complex.
Mechi ya mkondo wa kwanza nchini Botswana ilimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 kabla ya Yanga kushinda mabao 2-1 dimba la nyumbani.
Haukuwa mchezo mwepesi lakini wachezaji wa Yanga walionyesha kwa kiasi gani wako tayari kupambania malengo ya timu na hata ndoto ya kocha wao Manqoba ambaye ameonyesha imani kubwa kwao.
Yanga ilikuwa na wachezaji 11 uwanjani lakini kulikuwa na ushirikiano mkubwa baina yao na wenzao walio nje.
Mara kadhaa wachezaji kama Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' na hata Stephane Aziz Ki na Shalulile walipotoka waliendelea kusimama kuwaelekeza wenzao.



Ni wazi eneo la kwanza ambalo Manqoba amefanikiwa mapema ni kujenga umoja na ushirikiano miongoni mwa wachezaji wake.
Wachezaji wameonyesha umoja, yeyote anayepewa jukumu la kuanza kwenye kikosi anaungwa mkono kwa asilimia 100 na wenzake.
Hii ni timu ambayo wachezaji wanashirikiana na wako kitu kimoja katika kuhakikisha wanafanikisha jambo lao. Hatua ya kwanza ya mafanikio inaanza kwa kujenga timu, benchi la ufundi tayari limeonyesha kufanikiwa hapo.
ushindi wa Yanga sasa sio suala la mtu mmoja, kila mchezaji awe ndani au nje ya uwanja anafahamu wajibu wake na anashiriki vilivyo ili timu ipate ushindi.
Lakini pia uongozi chini ya Rais Injinia Hersi Said wako bega kwa bega na timu kila mara. Ni nadra sana kuiona Yanga ikicheza bila uwepo wa Hersi au Arafat pale uwanjani.
Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakitimiza wajibu wao kwa kiasi kikubwa. Yanga haijatawala soka la Tanzania kwa misimu mitano mfululizo kwa bahati mbaya. Sapoti ya mashabiki imeendelea kuwa chachu kubwa ya mafanikio hayo.
Msimu huu Yanga imeweka malengo makubwa kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa, kwa umoja na ushirikiano uliopo baina ya pande zote, hakuna lisilowezekana.
Misimu mitatu iliyopita Yanga ilicheza fainali ya kombe la Shirikisho la CAF (CAFCC) hakuna aliyewapa Wananchi nafasi ya kufikia mafanikio hayo lakini iliwezekana.