Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold umedhihirisha 'tabia ya kibingwa' ya Yanga kupata matokeo mazuri hata katika mechi ngumu.
Mchezo huo uliopigwa uwanja wa KMC Complex Jumanne usiku, uliwashuhudia Wananchi wakicheza zaidi ya dakika 75 wakiwa pungufu baada ya kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki kupewa kadi nyekundu mapema kwenye kipindi cha kwanza.
Kamwe amesema kadi nyekundu hiyo ilivuruga mipango ya Yanga kwenye mchezo huo lakini upambanaji na kujituma kwa wachezaji kuliwawezesha kushinda mchezo huo na kujihakikishia kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi.
"Tulianza mchezo vizuri lakini ni wazi kadi nyekundu aliyoonyeshwa Stephane Aziz KI ilibadilisha kwa kiasi kikubwa mpango wa timu."
"Benchi la ufundi walilazimika kubadili mfumo baada ya kupoteza mchezaji muhimu katikati ya uwanja. Lakini licha ya changamoto hiyo na pamoja na ubora wa Geita Gold, tulionyesha tabia ya kibingwa kwa kupambana hadi mwisho na kuondoka na pointi tatu"
"Kipekee kabisa, niwapongeze wachezaji wetu kwa kupambana na kulinda nembo ya klabu," alisema Kamwe
Ushindi huo ulikuwa na maana kubwa kwa Yanga kwani umewahakikishia Wananchi kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya mchezo dhidi ya watani zao Simba utakaopigwa Oktoba 10 baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.