Baada ya watani zao Simba kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa dabi ya Kariakoo utakaopigwa Oktoba 10, mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga wao hawana mpango wa kuondoka nchini wakitarajiwa kuendelea na maandalizi yao Avic Town.
Baada ya ligi kusimama, wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko ya siku 9 ambapo wanatarajiwa kurejea mazoezini siku ya Jumatatu kuanza maandalizi ya mchezo huo pamoja na mechi nyingine zitakazofuata.
Kwa misimu ya karibuni Yanga imeachana na utaratibu wa kwenda kufanya maandalizi nje ya nchi au hata nje ya jiji la Dar es salaam wakijichimbia Avic Town.
Misimu minne kati ya mitano ambayo Yanga imetwaa taji la ligi kuu mfululizo, Wananchi wamefanya pre-season Avic Town na hawajawahi kutoka hata pale wanapokutana na watani zao.
Katika kipindi chote Yanga imepoteza mchezo mmoja tu kwenye ligi dhidi ya Simba, April 16 2023 sasa ikipita zaidi ya miaka mitatu bila kupoteza mchezo dhidi ya Simba kwenye ligi kuu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesisitiza kuwa kikosi kitafanya maandalizi yake kama wanavyofanya siku zote na wana matumaini makubwa ya kushinda mchezo huo dhidi ya Simba.
Ikumbukwe Yanga na Simba zilikutana visiwani Zanzibar ufunguzi wa msimu huu kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kuelekea mchezo huo pia Wananchi walitokea Avic Town wakati watani zao walitokea Rwanda ambako walishiiriki michuano ta CECAFA Kagame Cup na kufanya maandalizi yao ya msimu.