Mabingwa wa kihistoria wa soka nchini, klabu ya Yanga SC, kwa kushirikiana na kampuni ya Safari Lager, wamezindua rasmi msimu wa tatu wa kampeni kubwa ya kusaka na kuibua vipaji vya soka nchini inayojulikana kama ‘Safari Lager Cup’.
Ushirikiano huo unaolenga kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji vya soka kutoka maeneo mbalimbali nchini, msimu huu utafanyika katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, na Arusha.
Kampeni hii inawalenga vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 23 ambao hawajapata fursa ya kucheza soka la ushindani katika ngazi za juu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu wa Yanga SC Andre Mtine alieleza kuwa mashindano haya ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuwekeza kwenye soka la vijana na kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao za kucheza soka la kulipwa.
Vijana watakaofanya vizuri watapata fursa ya kuonekana na makocha wa Yanga na hata kusajiliwa kwenye timu ya vijana ya klabu hiyo.
Kwa upande wa Safari Lager, wadhamini wakuu wa kampeni hiyo, walisisitiza kujitolea kwao kuendeleza michezo nchini na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kusajili timu zao kupitia ofisi za vyama vya soka katika mikoa husika ili kuonyesha uwezo wao na kuibua vipaji vipya vitakavyolisaidia taifa hapo baadaye.