Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesisitiza matumizi ya vifaa maalumu vya kupima ubora wa hewa (Gas Detectors) katika vyumba vya kubadilishia nguo za wachezaji wakati wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 9, 2026, TPLB imeeleza kuwa vifaa hivyo vitatumika kukagua vyumba vya kubadilishia nguo ili kuhakikisha ubora wa hewa na usalama wa wachezaji, benchi la ufundi pamoja na maafisa wa timu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukaguzi utaanza mara baada ya vyumba vya kubadilishia nguo kukabidhiwa kwa timu husika na utaendelea hadi mchezo utakapokamilika. Hatua hiyo inalenga kupima uwepo wa gesi ya oksijeni na hewa isiyo ya kawaida inayoweza kuhatarisha afya na usalama wa watumiaji wa vyumba hivyo.
TPLB imesema matumizi ya vifaa hivyo yalianza Oktoba 8, 2026, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kiusalama unaotekelezwa katika viwanja vyote nchini vinavyotumika kwa michezo ya ligi.
Bodi imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha vyumba vya kubadilishia nguo vinakuwa katika mazingira salama na yanayofaa kwa timu, huku afya na usalama wa wachezaji vikipewa kipaumbele.
Aidha, TPLB imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inafanyika katika mazingira salama, kwa kuzingatia taratibu na viwango vya usalama vinavyotakiwa.
Hatua hiyo inakuja katika kipindi ambacho Bodi inaendelea kuimarisha usimamizi wa masuala ya usalama viwanjani ili kulinda afya za wachezaji, benchi la ufundi na wadau wengine wa soka nchini.