Hatimaye ile siku imewadia! Ni Kariakoo Derby Simba na Yanga zikikutana kwa mara nyingine kwenye mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Timu hizo zinakutana tena 'Shamba la Bibi' baada ya kupita tkribani miaka 9 mara ya mwisho timu hizo zilikutana uwanja wa Uhuru mwaka 2017 mchezo ukimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1.
Kwenye mchezo huo Simba walitangulia kufunga kupitia Shiza Kichuya kabla ya Yanga kusawazisha kupitia Obrey Chirwa.
Leo ni siku nyingine tena kwa miamba hiyo ya soka nchini kukutana tena kwenye uwanja ambao umefanyiwa maboresho makubwa kuelekea michuano ya Afcon 2027 itakayofanyika nchini.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kibabe msimu huu ikishinda mechi zote sita za kwanza za ligi na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya mabao.
Wapinzani wao Simba nao wameshinda mechi zote sita pia lakini Yanga iko kileleni ikiwa na faida ya kufunga mabao matano zaidi.
Ni wazi itakuwa mechi ngumu kwani msimu huu kila timu imejipambanua na kuonyesha ubora.
Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi amekiri mchezo huo hautakuwa mwepesi lakini amesisitiza kuwa wamefanya maandalizi bora ya kimkakati ili kuhakikisha wanaondoka na alama tatu.
Utakuwa mchezo wa pili kwake kukutana na Simba baada ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa August 12 uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Kuelekea mchezo huo, Yanga wameonyesha utulivu mkubwa katika maandalizi yao wakigoma kujibu tambo za wapinzani wao Simba ambao wamepania kumaliza uteja kwa kushinda mchezo huo.
Matarajio ya mashabiki wa Yanga ni kuona timu yao inaendeleza ubabe dhidi ya Simba na mwanzo mzuri wa msimu ili kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi.
Kila la kheri Wananchi...!