Mengi yatasemwa lakini mwisho wa siku Wanayanga wanapaswa kukubali, Simba walikuwa bora sana kila idara wakionekana kuitaka mechi zaidi kuliko wachezaji wa Yanga.
Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi anaweza kulaumiwa kwa sababu ni yeye aliyepanga wale wanaume 11 walioingia uwanjani kuipambania Yanga kwenye mchezo huo waliokubali kipigo cha mabao 2-1.
Lakini kwa tathmini ndogo tu unaweza kuona leo Yanga ilizidiwa sio kimbinu tu bali kwenye utimamu wa kimwili wa wachezaji.
Ukiangalia takwimu za mchezo huo zinakuonyesha Yanga hawakukimbia sana kama walivyofanya Simba. Kwa mara ya kwanza leo wamemiliki mchezo chini ya asilimia 40, hii ni mechi ya kwanza kwa Yanga kucheza chini ya kiwango kiasi hicho msimu huu.
Kwa dakika zote 90 za mchezo Yanga imepiga mashuti mawili tu yaliyolenga lango huku Simba wakipiga mashuti 6 on target. Yanga ilitengeneza nafasi kubwa tatu tu wakati Simba walitengeneza nafasi 14.
Kipindi cha pili wachezaji wa Yanga walionekana kuwa wamechoka zaidi, wakilazimishwa kukaa nyuma kwa muda mwingi kwani hata mipira ilipopelekwa mbele haikukaa.
Ikumbukwe idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga (10) walikuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa na wengine wamerejea siku mbili kabla ya mchezo huo.
Haiwezi kuwa sababu pekee iliyopelekea Yanga kupoteana lakini ni wazi baadhi yao walikuwa na uchovu na pengine ndio maana hawakutoa uwezo wao kwa asilimia 100.
Sio suala la Yanga kupoteza leo lakini ni wazi timu haikuwa katika kiwango bora cha ushindani, pengine hapa ndipo uongozi na benchi la ufundi wanapaswa kuanzia.