Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeanza utaratibu wa kuwapima wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya pamoja na dawa zinazoweza kuongeza uwezo wa mwili kufanya vizuri zaidi michezoni.
Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema hatua hiyo inalenga kulinda uadilifu wa soka la Tanzania na kuhakikisha afya pamoja na usalama wa wachezaji vinapewa kipaumbele.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo suala la matumizi ya dawa zinazoweza kuongeza uwezo wa mwanamichezo limeimubua mijadala mitandaoni siku za karibuni .
Uamuzi wa kuanza utaratibu wa upimaji unalenga kuhakikisha kuwa wachezaji wanashindana kwa kuzingatia kanuni na taratibu za mchezo wa soka, bila kutumia njia zisizoruhusiwa zinazoweza kuwapa baadhi yao faida dhidi ya wengine.
Katika soka la ushindani, matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku yanaweza kuathiri afya ya mchezaji na kuleta maswali kuhusu uadilifu wa matokeo ya michezo.
Dawa za kusisimua misuli ni nini?
Dawa za kusisimua misuli na zinazoongeza uwezo wa mwili kufanya vizuri michezoni hujumuisha aina mbalimbali za vitu vinavyoweza kuathiri nguvu, uvumilivu au uwezo wa mwili kufanya kazi.
Hata hivyo, si kila dawa inayotumiwa na mwanamichezo imepigwa marufuku. Baadhi ya dawa hutumika kwa matibabu halali, lakini zinaweza kuhitaji tathmini maalumu kulingana na kanuni za kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku katika michezo.
Ndiyo maana upimaji na usimamizi wa kitaalamu ni muhimu ili kutofautisha matumizi yanayoruhusiwa kwa sababu za kiafya na matumizi yanayokiuka kanuni za michezo.
Afya za wachezaji kupewa kipaumbele
Mbali na kulinda ushindani wa haki, hatua hiyo ina umuhimu katika kulinda afya za wachezaji. Matumizi ya baadhi ya dawa bila usimamizi wa wataalamu yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa mwili, kutegemea aina ya dawa, kiasi kinachotumiwa na hali ya kiafya ya mhusika.
Kwa upande mwingine, utaratibu wa upimaji unapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia taratibu zinazotambulika, usiri wa taarifa za kiafya na haki za wachezaji wanaohusika.
Iwapo utaratibu huo utatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika, unaweza kusaidia kuongeza uwajibikaji katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kuimarisha imani ya mashabiki kuhusu ushindani wa haki.
Pia, unaweza kuongeza uelewa kwa wachezaji, makocha na madaktari kuhusu matumizi sahihi ya dawa na hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyoruhusiwa.