Mashabiki wa Yanga SC wamepata matumaini mapya kuhusu kurejea kwa kiungo mshambuliaji wao, Pacome Zouazoua, baada ya taarifa kueleza kuwa anaendelea vizuri katika hatua za kupona jeraha lililomuweka nje ya uwanja tangu mwezi Juni.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amefichua kuwa nyota huyo wa Ivory Coast anaendelea kuimarika na huenda akaanza rasmi mazoezi ya awali kabla ya Januari, endapo ataendelea vizuri na programu ya matibabu.
Akizungumzia maendeleo ya mchezaji huyo, Kamwe alisema Pacome kwa sasa anaendelea vizuri kiasi cha kuanza kuonekana uwanjani akiwaunga mkono wenzake wakati wa mechi na hata kutembelea mazoezini.
"Pacome anaendelea vizuri sana, sasa mnamuona anakuja uwanjani kushuhudia wenzake wakiipambania nembo ya Yanga na wakati mwingine mazoezini anafika," alisema Kamwe.
Aliongeza kuwa mchezaji huyo anatarajiwa kuingia katika programu ya pili ya matibabu yake hivi karibuni, ambayo itakapokamilika ataruhusiwa kuanza mazoezi ya awali kwa lengo la kurejesha mguu wake katika hali nzuri ya kiutendaji.
"Ataingia kwenye program ya pili ya matibabu yake karibuni ambapo program hiyo itakapokamilika ataanza rasmi mazoezi ya awali kurejesha mguu katika utimamu wake," alifafanua Kamwe.
Pacome amekuwa nje ya uwanja tangu mwezi Juni baada ya kupata jeraha kubwa lililohitaji kufanyiwa upasuaji.
Kukosekana kwake kumekuwa pigo kwa Yanga kutokana na mchango wake mkubwa katika eneo la ushambuliaji, hususan uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kucheza kwa kasi, kupenya kwenye safu za wapinzani na kufunga mabao.
Hata hivyo, hatua anazopiga katika matibabu zinaongeza matumaini kwa benchi la ufundi na mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.
Pacome ni miongoni mwa wachezaji waliopendwa na mashabiki wa Yanga kutokana na kiwango chake na mchango wake ndani ya kikosi.
Kutokana na umuhimu wake, kurejea kwake kutakuwa nyongeza muhimu kwa timu hiyo katika mapambano ya kuwania mataji ya msimu huu.