Wapinzani wa Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), MC Alger ya Algeria, wamefanya mabadiliko kwenye benchi lao la ufundi baada ya kuachana na kocha mkuu, Khaled Ben Yahia, siku chache kabla ya kukutana na Wananchi.
MC Alger wanatarajiwa kuvaana na Yanga Jumamosi, Novemba 28, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, katika mchezo wa kwanza wa Kundi B wa michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umefikia makubaliano ya pande zote mbili na Ben Yahia kusitisha mkataba wake, kufuatia kutokuwepo kwa maelewano kuhusu mwenendo wa timu katika Ligi Kuu ya Algeria.
MATOKEO YA LIGI YAMUANGUSHA
Inaelezwa kuwa uongozi wa MC Alger haujaridhishwa na mwenendo wa timu hiyo katika ligi ya ndani, ambapo inatajwa kushika nafasi ya tano kwenye msimamo, jambo lililochangia kufikiwa kwa uamuzi wa kuachana na kocha huyo.
Hatua hiyo imekuja katika kipindi ambacho MC Alger inajiandaa kuelekea mchezo wa ugenini dhidi ya Yanga, ambayo nayo inahitaji kuanza kampeni yake ya CAFCL kwa ushindi.
KOCHA MSAIDIZI APEWA MIKIMIKI
Kufuatia kuondoka kwa Ben Yahia, MC Alger inatarajiwa kuongozwa na kocha msaidizi Karim Belhum atakayeshika nafasi hiyo kwa muda katika mchezo dhidi ya Yanga..
Ni wazi mabadiliko ya kocha katika kipindi kifupi kabla ya mchezo mkubwa yanaweza kuathiri maandalizi ya timu hiyo na pengine kuipa faida Yanga kwenye mchezo huo wa kwanza kundi B.
Kwa upande wa Yanga, mchezo huo una umuhimu wa kipekee kutokana na kumbukumbu za kukosa nafasi ya kutinga robo fainali baada ya kulazimishwa sare tasa dhidi ya MC Alger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam misimu miwili iliyopita.