Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC, wameripotiwa kurejesha rada zao kwa kiungo mkabaji wa kimataifa wa Uganda, Bobosi Byaruhanga, wakilenga kumsajili katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari 2027.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa baada ya tathmini ya kina, uamuzi wa kuimarisha eneo la kiungo cha ukabaji umefikiwa ili kuongeza nguvu kwenye michuano ya ndani na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL).
Bobosi, mwenye umri wa miaka 24, anatajwa kama mtu sahihi wa kuongeza ushindani na mbadala thabiti katika eneo hilo ambalo katika dirisha lililopita Yanga ilimsajili Fredy Ngoma.
Kiungo huyo ambaye kwa sasa anakipiga kunako klabu ya Oakland Roots SC nchini Marekani, anatarajiwa kuwa mchezaji huru ifikapo Novemba 30, 2026, baada ya mkataba wake kumalizika.
Hali hiyo inaweza kuwapa Yanga urahisi wa kupata saini yake bila ya kulipa gharama kubwa kwa kuwa atakuwa mchezaji huru.
Hii si mara ya kwanza kwa miamba hiyo ya Jangwani kumtaka Bobosi. Yanga ilijaribu kumsajili miaka michache iliyopita alipokuwa aking'ara na Vipers FC ya Uganda kabla ya kutimkia nje ya nchi.
Duru za michezo zinanyapia kuwa nyota wa Uganda waliotamba na Yanga Khalid Aucho na Allan Okello wamekuwa wakitumika kwenye ushawishi kumvuta mchezaji huyo kujiunga na miamba hiyo ya soka la Afrika Mashariki.
Ikumbukwe pia upo uwezekano pia kwa Yanga kumrejesha Okello ambaye ameonyesha utayari wa kurejea tena Jangwani kutokana na changamoto ya kukosa nafasi kwenye klabu yakee ya sasa AS FAR.