Homa ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) kati ya Yanga na MC Alger ya Algeria imezidi kupanda visiwani Zanzibar, huku uongozi wa Wananchi ukiendelea na kampeni ya kuhamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mtanange huo.
Mapema leo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, akiambatana na maofisa kutoka Idara ya Wanachama ya klabu hiyo, ametembelea Tawi la Yanga la Mwembe Yanga, Makunduchi, Zanzibar, kwa ajili ya kufanya hamasa kuelekea mchezo huo.
Ziara hiyo imelenga kuhamasisha wanachama na mashabiki wa Yanga kununua tiketi mapema ili kuhakikisha Uwanja wa New Amaan Complex unajaa siku ya Jumamosi, Novemba 28, wakati Wananchi watakapowakaribisha MC Alger katika mchezo wa kwanza wa Kundi B.
Mbali na hamasa ya mchezo huo, Kamwe pamoja na maofisa hao wametumia fursa hiyo kuwahamasisha mashabiki kujisajili na kuwa wanachama hai wa Young Africans SC, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha msingi wa uanachama wa klabu hiyo.
OPERESHENI KUJAZA NEW AMAAN COMPLEX
Hamasa hiyo inakuja siku chache baada ya uongozi wa Yanga kutangaza viingilio vya mchezo huo, huku kiingilio cha chini kikiwa shilingi 5,000 na cha juu shilingi 30,000 kwa jukwaa la VIP.
Tiketi za mchezo huo zinapatikana kupitia mfumo wa Lipa Tiketi kwa kupiga msimbo 14946*11# au kutembelea tovuti ya http://yanga.lipatickets.tz/.
Uongozi wa Yanga unatambua umuhimu wa nguvu ya mashabiki katika michezo ya kimataifa, hasa katika pambano hili ambalo Wananchi wanahitaji kuanza kampeni yao ya hatua ya makundi kwa kuvuna pointi tatu muhimu.

