Methodi Mogella, fundi wa mpira ambaye pengo lake halijazibika

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
3 Sep 2018
Methodi Mogella, fundi wa mpira ambaye pengo lake halijazibika
Kwa wale 'wahenga' wanaofuatilia soka tangu miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya tisini, ukitaja jina la Method Mogella 'Fundi' lazima wajikute na huzuni wanapomkumbuka fundi huyu wa mpira aliyefariki akiwa na umri wa miaka 29 tu.

Method alifariki Novemba 12, 1994 ikiwa ni siku chache tu tangu arudi kutoka Arabuni alikokuwa amekwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa sambamba na Constanine Kimanda.

Method anakumbukwa zaidi kwa kuwa mmoja wa wanasoka waliocheza soka la mafanikio kwa ngazi ya klabu kiasi cha kuonekana mfano wa kuigwa akimudu vyema kucheza nafasi ya kiungo mchezeshaji.

Dimbani, Method alisifika kwa umahiri wake lakini nje ya uwanja Method alipendwa na kila mtu kutokana na tabia yake njema.

Alikuwa ni mchezaji ambaye umaarufu wake haukubadili chochote katika maisha yake nje ya soka.

Historia yake

Method alizaliwa mwaka 1965 mkoani Morogoro, alionyesha ana mapenzi makubwa na mchezo wa soka tangu alipokuwa anasoma katika shule ya msingi ya Msimbazi Boys wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wakati familia yake ilipokuwa inakaa Buguruni.

Katika miaka ya mwanzoni mwa 1980, nyota ya Method iliendelea kung'ara alipokuwa akisoma katika sekondari ya ufundi ya Mtwara akicheza nafasi ya kiungo na hata katika timu ya mtaani kwake Buguruni iliyofahamika kama Jay Ambe.

Alikuwa mwiba mkali kwa timu pinzani walizokutana nazo.

Lakini wakati Method akielekea kupata mafanikio katika soka, kulingana na makala iliyowahi kuandikwa na Shaffih Dauda, baba yake anayefahamika kwa jina la Martin Kunambi alikuwa hataki mwanaye ajihusishe na soka badala ya masomo hivyo alimpiga marufuku kucheza soka.

Hata hivyo juhudi za wanafamilia wengine akiwemo dada yake mkubwa aitwaye Angelina, zilisaidia kugeuza mtazamo wa baba yake kuhusu mwanaye kucheza soka.

Wakati Method akielekea kumaliza elimu ya sekondari baba yake alimruhusu kucheza soka kwa sharti la kujitengea muda wa masomo na michezo.

Jinsi alivyotua Simba kisha kusajiliwa na Yanga

Baada ya kumaliza elimu ya Sekondari, Method alijiunga na Chuo cha Ufundi Arusha ambako aliendelea kucheza soka kiasi cha kuitwa na timu za mitaani ili aweze kuzisaidia katika michuano mbalimbali.

Kutokana na kushiriki katika klabu mbalimbali za mtaani, Method aliweza kujulikana karibu katika eneo kubwa la Arusha kutokana na umahili wake katika kucheza soka.

Alipomaliza chuo na kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kama ilivyokuwa wakati huo kabla ya kurejeshwa kwa utaratibu huo hivi sasa, Method alijiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ambako aliendelea kucheza soka akiwa huko.

Akiwa katika kambi ya JKT, Meja Jenerali Makame Rashid alimuona Method akicheza soka na kuvutiwa naye ambapo haraka aliamua kumpeleka Dar es Salaam kujiunga na klabu ya Simba mwaka 1989.


Method Mogella (wa kwanza kushoto) akiwasalimiana na Waziri Mkuu John Malecela mwaka 1990

Akiwa Simba mwaka 1991, Methodi aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuifunga SC Villa kwa mabao 3-0 jijini Dar es salaam.

Method alisajiliwa na Yanga akitokea klabu ya Simba mwaka 1992, usajili wake ukifanikishwa na aliyekuwa mfadhili wa Yanga wakati huo Marehemu Abasi Gulamali.

Usajili wake wa kujiunga na Yanga ulikuwa gumzo kwani wakati huo Abasi aliyekuwa mfadhili wa Yanga alikuwa katika ushindani mkali na Azim Dewji wa Simba.


Method Mogella (wa nne kutoka kushoto) akiwa na kikosi cha Yanga mwaka 1993

Baada ya kuitumikia Yanga kwa msimu mmoja, msimu uliofuata Method aliipa masharti timu hiyo kuwa ili aweze kubaki Jangwani lazima Yanga imsajili mdogo wake Philothei Mogella.

Jambo hili linadhihirisha ni kwa kiasi gani Method aliwathamini watu wengine.

Method aliweza kutumia ushawishi wake kumsaidia mdogo wake aweze kusajiliwa moja kwa moja na Yanga.

Method alikuwa mmoja wa wachezaji wa kikosi cha Yanga kilichoshiriki kwa mafanikio michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1993.

Yanga ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo nchini Uganda kwa
kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yaliyofungwa na marehemu Said Mwamba Kizota na Edibily Lunyamila.

Muda mfupi baada ya kutwaa ubingwa huo, uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na mfadhili Gulamali uliamua kutoa zawadi ya seti ya televisheni na deki kwa kila mchezaji kama shukrani kwao kwa kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa huo.



Hivyo waliporejea nchini kutoka Uganda, Methodi na mdogo wake walizipeleka televisheni hizo nyumbani kwao Buguruni na kuifanya nyumba yao pekee kuwa yenye seti mbili za televisheni ambazo wakati huo zilikuwa adimu mitaani.

Mwaka 1994 baada ya kuonyesha uwezo mkubwa akiwa na Yanga, Method alisajiliwa na Malindi ya Zanzibar timu ambayo pia iliwasajili nyota wengine kama Edibily Lunyamila.

Baadae mwaka huo Method pamoja na beki kisiki aliyekuwa Yanga Constantine Kimanda waliitwa Uarabuni kwenda kufanya majaribio katika moja ya timu iliyokuwa inashiriki ligi kuu nchini humo.

Wakati Kimanda akifanikiwa, Method alilazimika kurudi nchini baada ya kufeli vipimo vya afya mwenyewe akibainisha kuwa aligundulika kuwa na matatizo ya macho.

Novemba 12 1994, Method alifariki dunia akiwa nyumbani kwa Baba yake Buguruni jijini Dar es salaam.

Siku moja kabla ya kifo chake, akiwa nyumbani kwake Mwenge, Method alilalamika kuwa na maumivu makali ya kichwa.

Tatizo hilo lilikuwa likimtokea mara kwa mara hali iliyopelekea siku hiyo Baba yake kuagiza arudishwe nyumbani kwao Buguruni kwa ajili ya uangalizi zaidi.

Method alilala kwao Buguruni na kuamka akiwa na hali nzuri.

Siku hiyo ambayo alifariki, asubuhi Method aliomba apikiwe viazi kama kifungua kinywa chake.

Lakini baadae Mama yake aliporejea chumbani kumletea kifungua kinywa alichoomba alimkuta amelala huko povu likimtoka mdomoni.

Haraka aliwaita watu waliokuwamo nyumbani hapo na kuwapeleka chumbani kumpa huduma ya kwanza.

Baada ya kuona hali si nzuri Method alikimbizwa hospitali ya Amana Ilala lakini ilibainika alikuwa tayari amefariki alipfikishwa Hospitalini hapo.
ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
34m ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
59m ago
READ MORE β†’
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
4h ago
READ MORE β†’
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
8h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
11h ago
READ MORE β†’
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
12h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
15h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
1d ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
1d ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’