Lwandamina kuamua ushindi wa Yanga

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
22 Aug 2017
Lwandamina kuamua ushindi wa Yanga
Ule mtanange wa watani wa jadi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu baina ya timu kongwe na zenye mashabiki wengi zaidi nchini Tanzania, Yanga na Simba unapigwa kesho Jumatano kwenye dimba la Taifa.

Mchezo huo wa Ngao ya Jamii unapigwa kufungua pazia la msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom 2017-18, ukitarajiwa kuanza majira ya saa 11 jioni.

Ligi kuu ya Vodacom itaanza Jumamosi ijayo, August 26.

Timu zote zimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo unaokuwa na kila aina ya ushindani ndani na nje ya uwanja.

Simba iliweka kambi ya wiki kadhaa nchini Afrika Kusini kisha kurejea jijini Dar es salaam na baadae kuelekea visiwani Zanzibar kabla ya kurejea tena Dar hapo jana.

Yanga iliweka kambi mkoani Morogoro na baadae kuelekea kisiwani Pemba na inarejea leo jijini Dar es salaam.

Mchezo huo ni muhimu sana kwa kila timu kupata ushindi kwani matokeo mabaya yanaweza kuiathiri timu itakayopoteza hasa ikizinagatiwa ligi itaanza siku tatu baadae.

Timu zote zimefanya usajili kambambe, kila timu inaamini ina kikosi bora zaid msimu huu hivyo ubora wa vikosi utaanza kupimwa katika mchezo huo.

Lakini tambo nyingi zaidi zimekuwa zikitolewa na Simba kupitia msemaji wa klabu hiyo Haji Manara na hata baadhi ya viongozi na mashabiki wa timu hiyo.

KWA NINI SIMBA INAJIAMINI SANA?

Simba imejipambanua kuwa imefanya usajili bora zaidi kuliko timu nyingine msimu huu.

Juzi kwenye mkutano Mkuu wa klabu hiyo, uongozi ulitoa taarifa kuwa klabu imetumia takribani Bil 1.3 kwa usajili kuanzia dirisha dogo.

Hivyo ni dhahiri matokeo mengine tofauti na ushindi yatapelekea msuguano baina ya wadau wake na pengine kupelekea timu hiyo kuboronga zaidi kwenye ligi.

Kwani miongoni mwao wapo wanaohoji usajili wa baadhi ya wachezaji ambao wengine tayari ni majeruhi hata kabla ya ligi kuanza.

Hawa watapaza sauti zao zaidi kama Simba itafungwa katika mchezo huo.

YANGA TULIIIVU

Moja ya mapinduzi makubwa yaliyofanywa na uongozi wa Yanga tangu kuingia kwa Katibu Mkuu Charles Mkwasa ni aina ya ufanyaji kazi wa klabu hiyo.

Yanga imeachana na mtindo wa tambo za majukwaani na kupiga makelele kama ilivyo kwa wapinzani wao.

Sijawahi kumsikia msemaji wa klabu ya Yanga Dismas Ten akijigamba kuhusu timu yake zaidi amekuwa akitoa taarifa stahiki kwa wadau wa Yanga pale inapohitajika.

Hii imewafanya WanaYanga wawe wamoja zaidi na kuwa nyuma ya timu yao. Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na utulivu kuanzia kwa wachezaji na hata mashabiki wake.

Matokeo mabaya hayawezi kuivuruga Yanga kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wapinzani wao Simba ambao wataingia dimbani wakiwa na matokeo ya USHINDI mfukoni.

Mashabiki wa Simba hawajaandaliwa kisaikolojia iwapo timu yao itafungwa wakubali matokeo. Kwani mpira wa miguu una matokeo matatu tu, kushinda, kufungwa au sare.

Na Kama hili likitkea haitakuwa mara ya kwanza, msimu uliopita mashabiki wa Simba walifanya uharibifu kwenye dimba la Taifa kutokana na tabia ya viongozi wao kuwaaminisha kuwa timu yao haiwezi kufungwa na Yanga.

KIUFUNDI, TIMU HAZITOFAUTIANI SANA

Ukiangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kutoka timu zote, hakuna tofauti kubwa sana. Hivyo makocha wana nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya mchezo huo kulingana na jinsi watakavyopanga vikosi vyao na mifumo watakayotumia.

Hata hivyo ni kocha wa Yanga George Lwandamina mwenye nafasi zaidi ya kuamua matokeo ya timu yake kwenye mchezo huo kwa kuwa tayari anafahamu saikolojia ya wapinzani wake.

Kama nilivyosema awali, licha ya usajili wa 'mabilioni' uliofanywa na Simba, bado timu hiyo imeonekana kuwa na matatizo kwenye safu ya ushambuliaji.

Kabla ya mchezo wao dhidi ya timu dhaifu ya Gulioni, Katika michezo mitano ya kirafiki iliyocheza Simba ilikuwa imefunga mabao matatu pekee.

Hivyo ni dhahiri katika mchezo huo Simba itauanza kwa kasi kujaribu kusaka mabao ya haraka haraka. Lwandamina ni lazima afahamu kikosi chake kinaweza kuwa na wakati mgumu kwenye dakika za mwanzo za mchezo huo.

Ni Lazima aanze na mfumo ambao utakuwa na uwiano mzuri wa wachezaji kukabiliani na mashambulizi ya Simba mwanzoni mwa mchezo.

Kwenye michezo yake mingi ya kirafiki kocha wa Simba Joseph Omog amekuwa akitumia zaidi mfumo wa 4-2-3-1.



Simba itawatumia zaidi wachezaji wake wa pembeni Zimbwe Jr, Okwi, Shomari/Nyoni na Shiza Kichuya kupeleka mashambulizi kwenye lango la Yanga.

Niyonzima atakuwa na majukumu ya kuhakikisha washambuliaji wanapata mipira sahihi.

Hivyo Lwandamina anahitaji kuwa na walinzi wa pembeni na viungo wa kati mahiri watakaoweza kwenda na kasi ya mashambulizi ya Simba.

Kocha Lwandamina hupendelea kutumia mfumo wa 4-4-2, na hata kwenye michezo kadhaa ya kirafiki ametumia mfumo huo huku mara chache akitumia 4-3-3 au 4-1-4-1.

Hata hivyo mfumo wa 4-4-2 unaweza ukamuangusha kwenye mchezo huo kwani mfumo huo unaweza kutoa nafasi kwa Simba kutawala sehemu ya kati kwa kuwa itakuwa na viungo wengi.



Akitumia mfumo unaoshabihiana na Simba au hata hiyo 4-1-4-1 ataweza kudhibiti sehemu ya kiungo lakini itamlazimu atumie wachezaji wenye umahiri zaidi ya kukaba.



Uzuri wa kikosi cha Yanga wachezaji wake wana stamina ya hali ya juu, majuzi tu tumemsikia kocha wa Mlandege ambaye timu yake ilicheza mchezo wa kirafiki na Yanga akikiri alifungwa kutokana na stamina ya wachezaji wa Yanga kuwa juu.

Pia kocha huyo akafunguka kuwa ilikuwa rahisi kuidhibiti Simba kwa kuwa stamina ya wachezaji wa kikosi chao haikuwa sawa.

Hivyo kama kikosi cha Lwandamina kitafanikiwa kuidhibiti Simba isipate bao katika dakika 20 za mwanzo, basi upo uwezekano mkubwa wa Yanga kuondoka na ushindi kwenye mchezo huo.

Pia bado Yanga ina safu bora ya ushambuliaji kuliko Simba. Washambuliaji Donald Ngoma, Ibrahim Ajib na Amissi Tambwe wanayo nafasi ya kuibeba Yanga kwenye mchezo huo.

Aidha takwimu zinaonyesha Yanga haijawahi kupoteza mchezo dhidi ya Simba Ngoma anapokuwa dimbani.
ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
2h ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
2h ago
READ MORE β†’
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
5h ago
READ MORE β†’
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
10h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
13h ago
READ MORE β†’
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
14h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
16h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
1d ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
1d ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’