Kesi ya Manji yaendelea Kisutu

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
23 Aug 2017
Kesi ya Manji yaendelea Kisutu
Kesi ya Mfanyabishara na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga Yusufali Manji inaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.

Hapo jana Shahidi wa kwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Ramadhani Kingai (41), aliiambia Mahakama kuwa aliagiza mfanyabiashara Yusufali Manji apelekwe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ili akapimwe sampuli ya mkojo wake na majibu yalionyesha kuwa na chembechembe za dawa za kulevya.

Kadhalika, amedai kuwa aliagiza Manji akapimwe kwa sababu alikuwa anatuhumiwa kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Kingai alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis, shahidi huyo wa Jamhuri alidai kuwa Februari 9, mwaka huu, Manji alifika kujisalimisha baada ya kutajwa kwenye orodha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam dhidi ya tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Alidai kuwa aliteuliwa kama mwenyekiti wa kufanyia kazi taarifa za mkuu wa mkoa kuhusu watuhumiwa wa dawa za kulevya.

Shahidi huyo ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alikuwa mwenyekiti wa uchunguzi wa watuhumiwa wote waliohusishwa na dawa za kulevya.

Alidai baada ya kumhoji mshtakiwa na kujiridhisha, aliagiza apelekwe kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kupimwa sampuli ya mkojo wake.

"Kwa sababu Manji alikuwa anatuhumiwa kufanya biashara na kutumia dawa za kulevya, nilimwagiza Koplo Sospita ampeleke kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kupimwa sampuli za mkojo wake... agizo langu lilitekelezwa," alidai shahidi.

Alidai kuwa akiwa kama mwenyekiti wa uchunguzi huo, baada ya Manji kupimwa majibu yalionyesha anatumia dawa za kulevya.

"Baada ya majibu kuonyesha kuwa anatumia dawa za kulevya niliagiza afunguliwe jalada la makosa ya jinai, lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) na alipojiridhisha alifunguliwa mashtaka."

Naye shahidi wa pili, Koplo Sospita (49), alidai kuwa siku ya tukio alipewa maelekezo na Kindai ya kumpeleka Manji kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kupima sampuli ya mkojo.

Alidai kuwa alipofika katika ofisi hiyo alikabidhiwa kontena maalum kwa ajili ya kuwekea sampuli ya mkojo na mshtakiwa alifanya hivyo.

Alidai kuwa baada ya kumkabidhi mtaalamu Lucian Dominic, alirejea siku ya pili yake Februari 10, kwa ajili ya kupata majibu ya sampuli hiyo.

"Nilipokea majibu, nilipoyasoma niliona yameandikwa mkojo wa Manji umebainika kuwa una chembechembe za dawa za kulevya," alidai shahidi.

Kesi hiyo inaendelea leo kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, unatarajia kuita jumla ya mashahidi 10 kuthibitisha kosa dhidi ya mfanyabiashara huyo wa jijini Dar es Salaam.

Katika kesi ya msingi, Vitalis alidai kuwa Manji ni mfanyabiashara maarufu nchini, anakabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa za kulevya.

Alidai kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View, jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Vitalis alidai kuwa mshtakiwa ni mkazi wa Upanga jijini Dar es Salaam.

Manji ambaye pia ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mbagala, alikiri anuani yake na kwamba ni kweli yeye ni mfanyabiashara, lakini alikana kutumia dawa za kulevya.

Mbali na kesi ya kutumia dawa za kulevya, Manji (41) anakabiliwa na kesi nyingine ya mashtaka ya uhujumu uchumi mahakamni hapo.

Katika kesi hiyo, inadaiwa Manji na wenzake watatu, pamoja na makosa mengine walikutwa na vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Kosa la uhujumu uchumi halina dhamana kisheria mpaka kwa ruhusa ya Mahakama Kuu hivyo, Manji amebaki kuwa gerezani.
ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
1h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
3h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
7h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
16h ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
21h ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
1d ago
READ MORE β†’
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
1d ago
READ MORE β†’
Droo ya makundi CAF ni Jumatano
Droo ya makundi CAF ni Jumatano
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
1d ago
READ MORE β†’