Licha ya msimamo mkali wa kocha Mwinyi Zahera kuhusu mlinda lango Beno Kakolanya, uongozi wa Yanga unafanya jitihada ya kumaliza tofauti iliyojitokeza ili mlinda lango huyo aweze kurejeshwa kikosini.
Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakutaka jina lake liwekwe hadharani amesema jitihada za kumrejesha Beno kikosini zinafanyika.
"Kakolanya bado ni mchezaji mwenye mkataba na Yanga hivyo ni mchezaji wetu halali licha ya sintofahamu iliyojitokeza siku za karibuni, " amesema
"Jitihada zinafanyika ili kumaliza tofauti iliyojitokeza. Tunasubiri kocha arudi tufanye kikao kitakachohusisha viongozi wa Yanga, Beno na Kocha Mwinyi Zahera ili kupata suluhu ya jambo hili"
"Baada ya kikao hicho maamuzi yatakayofikiwa tutawajuza Wana Yanga"
Kwa sasa Yanga inawategemea makipa wawili Ramadhani Kabwili na Klaus Kindoki wakati usajili wa kipa mpya Ibrahim Hamid ukipingwa na kocha Zahera aliyesema viongozi wa Yanga walimsaji mlinda lango huyo bila ya ruhusa yake.
Juzi mkoani Arusha kwenye mchezo wa ligi dhidi ya African Lyon Kabwili alipata majeraha ya nyonga yaliyopelekea akimbizwe Hospitalini kufanyiwa vipimo zaidi na baadae kuruhusiwa.
Kama Kabwili (ambaye inaelezwa hali yake inaendelea vizuri) atashindwa kurejea langoni mapema basi Yanga itamtegemea mlinda lango mmoja, Klaus Kindoki.
Hapo ndipo ulazima wa kumrejesha Kakolanya kikosini unapojitokeza.
Mashabiki wamtaka aombe radhi, asamehewe
Katika hatua nyingine baadhi ya mashabiki wa Yanga wamemtaka mlinda lango Beno Kakolanya kumuomba radhi kocha Mwinyi Zahera, uongozi wa Yanga, wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwa uamuzi wake wa kugoma wakati timu hiyo ikimuhitaji.
"Yanga inamuhitaji Beno na yeye pia anaihitaji Yanga. Bila shaka atakuwa amejifunza. Ni vyema akajitokeza hadharani kuiomba radhi familia ya Wana Yanga ili aweze kusamehewa," amesema shabiki aliyejitambulisha kwa jina moja la Rashidi
"Hatuna shaka na uwezo wake. Naamini bado anahitajika sana kwenye kikosi cha Yanga. Atumie changamoto iliyojitokeza kujitafakari na kama atarejeshwa kikosini asirudie makosa"
Hivi karibuni Wakala wa mlinda lango huyo Seleman Haroub aliutaka uongozi wa Yanga kumaliza sintofahamu iliyojitokeza ili mteja wake aweze kurejea kazini kwani changamoto ya kutocheza imeanza kumuumiza kisaikolojia
Licha ya kumsimamia Beno, Haroub ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba.
Moja ya mambo ambayo hayakumfurahisha kocha Zahera ni hilo la mchezaji wake kusimamiwa na kiongozi wa klabu ya Simba.