Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewasili Alfajiri ya leo Alhamisi, Disemba 27 na ataungana na kikosi cha timu hiyo ambacho tayari kiko mkoani Mbeya kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.
Mchezo huo utapigwa kwenye dimba la Sokoine keshokutwa Jumamosi, Disemba 29 2018.
Baada ya kutua Zahera amesema timu inaelekea mkoani Mbeya ikiwa na lengo la kupata matokeo ili iweze kukamilisha mzunguuko wa kwanza ikiwa inaongoza ligi.
"Program ya mazoezi nilimuachia Kocha Noel na nafurahi kuwa ilifanyika vizuri," amesema Zahera
"Nimezungumza na wachezaji, wanafahamu umuhimu wa mchezo dhidi ya Mbeya City. Lengo letu ni kumaliza mzunguuko wa kwanza tukiwa tunaongoza ligi"
Kocha Zahera pia amewapongeza mashabiki wa Yanga kwa kufanikisha safari ya Mbeya ya kikosi cha timu hiyo.
"Tunawashukuru sana mashabiki na wanachama wetu kwa msaada wao kwetu sisi tunawaahidi kuwapa furaha ya ushindi kwenye kila mchezo utakao kuwa mbele yetu Mungu atusaidie sana na awabariki wote"
Akiwa nchini Ufaransa Zahera aliwahamasisha Wana Yanga kuichangia timu ili iweze kupata fedha za kugharamia usafiri wa ndege wa timu yao kuelekea mkoani Mbeya.