Wakati mwingine kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera anapewa lawama asizostahili kwa kukataa kumpokea mlinda lango Beno Kakolanya.
Beno alimkosea Zahera, aliwakosea wachezaji wenzake na Wana Yanga wote kwa kukiuka makubaliano aliyokuwa ameyaafiki ili kulinda maslahi mapana ya Yanga.
Cha kushangaza Beno amekuwa akiombewa msamaha na watu wengine, kwa nini asiifanye hiyo kazi yeye mwenyewe ili kuonyesha kweli anahitaji msamaha?
Kuna ugumu gani kwa Beno kuwaomba radhi wachezaji wenzake, kocha, uongozi wa Yanga na wadau wote wa klabu hiyo?
Miaka ya nyuma Yanga iliwahi kumfungia aliyekuwa kiungo wake wakati huo Haruna Niyonzima kutokana na masuala ya utovu wa Nidhamu.
Niyonzima aliupigania msamaha wake kwa kujitokeza hadharani na kuomba radhi. Alisamehewa na umaarufu wake ukazidii kuongezeka miongoni mwa Wana Yanga.
Ukifuatilia kwa umakini utabaini Zahera yuko sahihi kabisa kwa msimamo aliouweka juu ya Beno kwani yeye mwenyewe haonekani kufanya jitihada zozote ili aweze kusamehewa.
Pengine umaarufu alioupata msimu huu baada ya kuonyesha kiwango cha juu anadhani hastahili kujishusha.
Ikumbukwe Beno aliiacha Yanga usiku wa manane wakati inajiandaa kucheza na Ndanda FC. Kocha Zahera ni miongoni mwa waliomshawishi bila ya mafanikio mlinda lango huyo asiondoke kambini
Mbaya zaidi inadaiwa Beno alifuatwa na Meneja wake usiku huo na siku chache baadae wakajaribu kuishinikiza Yanga ivunje mkataba wake bila ya mafanikio.
Tuhuma za kuwa Beno alikuwa akitumiwa na Meneja wake kwa maslahi ya Simba zinaweza kuwa na mashiko hasa ukifuatilia mwenendo wa Meneja wake huyo ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba.
Kwani kama ingekuwa ni uamuzi wa mchezaji mwenyewe naamini Beno angejitokeza hadharani na kuomba radhi.