Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga leo wanashuka uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar kuikabili Azam Fc kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi, kundi B
Katika mchezo wake wa kwanza, Azam Fc ililazimishwa sare ya bao 1-1 wakati Yanga iliilaza KVZ kwa bao 1-0 na kuchupa kileleni mwa kundi hilo
Ni mchezo ambao umevuta hisia za wakazi wa Zanzibar kutokana na unazikutanisha timu ambazo ni bora na zinafuatana kileleni katika mbio za ubingwa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Tofauti na Yanga, Azam Fc ilikwenda Zanzibar ikiwa na kikosi chake kamili kilichosheheni nyota wake wote.
Hali ndio inayompa kiburi kocha Mkuu wa timu hiyo Hans van Pluijm ambaye amesema anahitaji kushinda mchezo huo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali.
Licha ya kikosi chake kusheheni wachezaji wa timu ya vijana, Yanga sio timu ya kubeza kwenye michuano hiyo kwani ndio timu pekee iliyopata ushindi kundi B kwenye michezo ya raundi ya kwanza.
Kocha Noel Mwandila amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na hawaihofii timu yoyote kwenye michuano hiyo ikiwemo Azam Fc.