Kiungo Mohammed Issa 'Banka' amebakisha takribani wiki tatu tu amalize adhabu yake ya miezi 14 aliyofungiwa na FIFA kutokana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku michezoni.
Banka ataanza rasmi kuvaa uzi wa Yanga February 08 2019 adhabu yake itakapokuwa imemalizika.
Lakini tangu mwezi uliopita mchezaji huyo aliruhusiwa kujifua na kikosi cha Yanga kujiweka sawa kabla adhabu yake haijamalizika na kurejea dimbani.
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ameeleza kuvutiwa na kiungo huyo akimsifu kuwa ni aina ya wachezaji anaopenda kufanya kazi nao.
Muda mfupi aliofanya nae mazoezi Zahera amebaini kiungo huyo atakuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha Yanga ambacho sasa kimeweka dhamira ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
"Nimevutiwa sana na Banka ukimuona uwanjani mazoezini utagundua kwamba ni mchezaji ambaye licha ya kuwa nje kwa muda mrefu lakini alikuwa akizingatia nidhamu ya mwili, nilikuwa nahitaji sana mtu kama huyu katika timu yangu, " Zahera amenukuliwa na MwanaSpoti
Zahera amesema katika mazoezi ya Yanga Banka ameonyesha uwezo mkubwa katika majukumu ya ukabaji, kuchezesha timu na hata kufunga vitu ambavyo vitaipa nguvu timu yake katika mzunguko wa pili