Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imebakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Uganda ambao inahitaji kushinda ili kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 zitakazopigwa mwezi Juni nchini Misri
Mchezo huo utapigwa mwezi March sambamba na mchezo wa Cape Verde dhidi ya Lesotho. Kama Stars itaifunga Uganda na Lesotho ikashindwa kupata ushindi ugenini dhidi ya Cape Verde, basi Stars itafuzu
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera anaamini Stars itafuzu kwa michuano ya AFCON 2019 akibainisha kuwa timu hiyo ina wachezaji wengi wenye vipaji kuliko Uganda.
Aidha Zahera amesema nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib ambaye sasa 'ameiva', anaweza kuisaidia Stars kushinda mchezo huo kama ataitwa na kocha Emmanuel Amunike
Zahera anaamini kazi anayoifanya Ajib kwenye kikosi cha Yanga ataifanya katika timu ya Taifa pia
Katika mabao 38 ambayo yamefungwa na Yanga kwenye ligi, Ajib amehusika kwenye mabao 20, akifunga mabao sita na kutengeneza nafasi za mabao 14
Kulingana na takwimu, Ajib ndiye mchezaji bora wa ligi kwa sasa kwani amekuwa chachu ya ushindi wa kikosi cha Yanga kila anapokuwa dimbani
Mashabiki wa soka nchini watakuwa na shauku kubwa kuona Ajib anaitwa katika kikosi cha Stars kitakachoivaa Uganda