Baada ya kushinda michezo 10 mfululizo, Yanga imepoteza mchezo wake wa pili katika kipindi cha siku nne
Jumamosi iliyopita ilichapwa bao 1-0 na Stand United katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara na leo imeondoshwa kwenye michuano ya SportPesa Cup kwa kufungwa mabao 3-2 na Kariobang Sharks ya nchini Kenya
Ukiacha suala la mlinda lango Klaus Kindoki ambaye bado anaonekana kukosa kujiamini, katika michezo ya hivi karibuni, safu ya ulinzi ya Yanga imeonekana kufanya makosa mengi
Mabao mawili kati ya matatu yaliyofungwa na K Sharks leo, wafungaji walikuwa huru kumtungua Kindoki
Mara kadhaa safu ya ulinzi ya Yanga inaonekana kukatika, timu haionekani kuwa na kiungo mkabaji.
Abdallah Shaibu ni beki mzuri lakini anapotumiwa kama kiungo mkabaji haleti tija kwa timu. Mara nyingi timu inaposhambuliwa hawi mahali anapaswa kuwa
Pia kiungo Haruna Moshi 'Boban' bado hajaweza kufanya kazi ambayo wengi walitarajia aifanye pengine majukumu anayopewa na Mwalimu yanamfanya asionekane
Makambo ndiye kinara wa mabao wa kikosi cha Yanga lakini kwenye mchezo wa leo ameinyima timu yake ushindi
Lengo la timu ni kushinda, hivyo wakati mwingine ni vyema kumpasia mwenye nafasi nzuri zaidi ya kufunga.
Moja ya nafasi alizopoteza katika mchezo wa leo angeweza kumpasia mpira mwenzake aliyekuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufunga
Hata hivyo matokeo ya mchezo wa leo hayapaswi kuwavuruga Wana Jangwani.
Sawa, wengi walikuwa na matumaini makubwa kwa timu kufanya vizuri lakini haikuwa.
Kariobang Sharks imeonyesha sio timu ya kubeza. Timu hiyo imeonyesha kuwa na wachezaji wazuri na haishangazi kusikia katika ligi kuu ya Kenya haijapoteza mchezo baada ya kushuka dimbani mara nane
Baada ya kuondoshwa kwenye michuano hiyo Yanga inapaswa kuelekeza nguvu zake kwenye ligi na michuano ya kombe la FA
Kocha Mwinyi Zahera ana takribani wiki nzima kusahihisha makosa ya kikosi chake kabla ya kwenda kuikabili Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara utakaopigwa Februari 02 mkoani Tanga