Kesi iliyofunguliwa Januari 11 na Wanachama wawili wa klabu ya Yanga, Juma Magoma na Athuman Nyumba kupinga mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi zilizowazi, imetajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es salaam.
Hata hivyo wadaiwa katika kesi hiyo, Bodi ya Wadhamini ya klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), hawakuwepo Mahakamani hivyo kesi hiyo itatajwa tena Februari 11 2019
Aidha baada ya Mawakili wa upande wa walalamikaji kumtaarifu Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega kuwa mlalamikiwa wa pili (Bodi ya Wadhamini ya Yanga) iligoma kupokea wito wa kuitwa Mahakamani, Mahakama imeamuru Bodi ya Wadhamini ya Yanga itangazwe gazetini kama njia ya wito wa kufika Mahakamani
Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, walalamikaji wanapinga kufanyika kwa uchaguzi wa kujaza nafasi zilizowazi katika klabu ya Yanga kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya klabu ya Yanga
Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahela alisema walikuwa wamefikia makubaliano na walalamikaji ili waiondoe kesi hiyo Mahakamani kuruhusu mchakato wa uchaguzi huo uweze kuendelea