Kabla ya kwenda mkoani Tanga kuikabili Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Januari 31 Yanga inakabiliwa na mchezo wa kombe la FA (ASFC) raundi ya tano dhidi ya Biashara Fc
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema mchezo huo una umuhimu wa kipekee kwa kikosi chake ambacho kimedhamiria kushiriki michuano ya Afrika msimu ujao
Zahera amesema Yanga imetoka kupoteza michezo miwili mfululizo, na haitakuwa tayari kupokea kipigo cha tatu
Amesema kama wataruhusu kupoteza mchezo huo dhidi ya Biashara watajiweka katika wakati mgumu na morali ya wachezaji itashuka huku wakijiweka kwenye nafasi ngumu ya kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.
"FA ni michuano mikubwa ambayo inatoa mwakilishi wa nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, malengo yetu ni kuchukua kombe hil, tunaendelea kujipanga ili tufikie mipango yetu," Zahera alinukuliwa na Nipashe
Hiyo itakuwa mara ya pili kwa Yanga kuchuana na Biashara Fc katika dimba la Taifa. Timu hizo zilikutana kwenye mchezo wa ligi na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1
Hata hivyo Yanga ililazimika kufanya kazi ya ziada ikitokea nyuma na kuibuka na ushindi huo