Kesho Jumatano Yanga itashuka dimba la CCM Kirumba kuikabili Mbao Fc kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara
Yanga iko mkoani Mwanza tangu jana leo ikitarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho kuelekea mchezo huo
Mbao Fc ina rekodi ya kipekee inapocheza na Yanga kwenye uwanja wake wa nyumbani kama ilivyo Yanga katika dimba la Taifa
Yanga haijawahi kuondoka na alama hata moja jijini Mwanza, Mbao Fc ikishinda michezo yote iliyopigwa CCM Kirumba tangu ilipopanda daraja misimu miwili iliyopita
Hata hivyo Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kesho watalifanya jambo hilo libaki historia. Kwani amekiandaa kikosi chake kikamilifu kuvunja mwiko huo na kuondoka na alama zote tatu
"Nimekuwa nikiwafuatilia Mbao Fc, wana timu nzuri. Wanacheza mpira mzuri pia wanafahamu kujilinda," amesema Zahera
"Nafahamu Yanga haijawahi kushinda dhidi ya Mbao Fc hapa Mwanza, nimewaambia vijana wangu kesho nataka ushindi. Tumefanya maandalizi ya kutosha naamini tutapata matokeo mazuri"
Mchezo wa kesho una umuhimu wa kipekee kwa Yanga ambayo baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba inahitaji alama tatu ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu