Mwenendo wa uchangia umemkatisha tamaa kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ambaye ametangaza kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu kama hakutakuwa na mabadiliko
Zahera amekuwa sehemu ya familia ya Yanga ambapo anajitoa na kutumia gharama kuhakikisha timu inafanikiwa
Alibuni mpango wa kuwashirikisha Wana Yanga kuichangia timu yao ili msimu ujao aweze kutengeneza kikosi imara
Hata hivyo mwenendo wa uchangiaji umekuwa mdogo hali iliyomkatisha tamaa Zahera kwani uwezekano wa kukusanya kiasi cha fedha zinazohitajika ni mdogo
"Kama mambo yataendelea hivi basi msimu huu ukimalizika nitaachana na Yanga kwa sababu tayari nimeshafanya mengi sana kwa ajili ya timu, naamini hakuna mtu atachukia kwa maamuzi yangu," amesema Zahera
"Nimewasaidia kwa vitu vingi ila naona kama vile wao wenyewe hawapendi kujisaidia, wanachama na mashabiki wa Yanga Tanzania wakumbuke ule msemo 'Ukijisaidia na Mungu atakusaidia'"
"Tuliwaambia wanachama na mashabiki tuijenge timu sisi wenyewe ila hakuna chochote kilichofanyika, mpaka sasa imepatikana sh 25 milioni tu, binafsi niliweka Milioni mbili na mimi si shabiki wala mwanachama. Yanga ina wanachama matajiri wengi sana ila nashindwa kuelewa kwanini hawachangii, kama kila tajiri angetoa milioni mbili tungeweza hata kununua wachezaji wazuri ifikapo Mei"
"Mashabiki na Wanachama wa Yanga waache kusema tu wanaumia timu ikifanya vibaya, badala yake waisaidie ifanye vizuri na kama hawataki basi wajue kwa upande wangu itakuwa ngumu sana kuendelea kujitolea kwa watu ambao hawajali"