Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema wanatambua timu ya Alliance Fc iko kwenye kiwango bora sana wakati huu ikiwa haijapoteza mchezo katika uwanja wake wa nyumbani tangu kuanza kwa mzunguuko wa pili, hivyo wataikabili timu hiyo kwa tahadhari kubwa
Yanga tayari iko mkoani Mwanza ikiwasili leo kwa usafiri wa Ndege kutoka jijini Dar es salaam
Saleh amesema mchezo wa keshokutwa hautakuwa na tofauti na michezo mingine waliyocheza ugenini, wanafahamu wenyeji watakamia mchezo huo lakini hilo haliwasumbui
"Alliance ni timu nzuri na hasa kwenye kipindi hiki cha karibuni, lakini sisi tunakwenda kucheza kama mechi zingine zote kwa sababu hizi timu za mikoani zote zinapocheza na Yanga na Simba zinacheza kwa kukamia sana, hili sisi tunalijua na tumejipanga kwa hilo," amesema Hafidh.
"Kikosi chetu hakina majeruhi wa kutisha wala kadi, hivyo Kocha Mwinyi Zahera, atakuwa na wigo mpana wa kuchagua timu anayotaka kuianzisha.
"Tunahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kuweka hai matumaini ya kurejesha ubingwa wetu. Bado mbio za ubingwa ziko wazi, timu yoyote ile kati ya sisi [Yanga), Simba na hata Azam, inaweza kushinda ubingwa"
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 61, alama 11 zaidi ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili na alama 13 zaidi ya Simba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na alama 48
Azam Fc na Yanga zote zimeshuka dimbani mara 25 huku Simba ikiwa imeshuka dimbani mara 19