Mshambuliaji wa AS Vita Club Jean Marc Makusu amekuwa katika kiwango bora kunako klabu hiyo iliyopangwa kundi moja na Simba katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, hatua ya makundi
Makusu ameifungia Vita Club mabao matano katika michunao hiyo msimu huu na kuwa miongoni mwa vinara wa upachika mabao
Tayari timu kadhaa zinaiwania sahihi yake kwa ajili ya msimu ujao ambapo mkataba wake na Vita unamalizika mwishoni mwa msimu
Miongoni mwa timu hizo ni Yanga inayonolewa na kocha Mwinyi Zahera, na klabu ya Simba ambayo mwekezaji wake ni Bilionea Mohammed Dewji 'Mo'
Awali ilikuwa ikielezwa Makusu ameshamalizana na klabu moja ya nchini Morocco, hata hivyo imebainika timu hiyo ilifanya nae mazungumzo ya awali tu
Inaelezwa Yanga inajipanga kumnasa Makusu kwa kutumia ushawishi wa Zahera ambaye anamnoa katika kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo
Kocha Msaidizi wa Vita Club Raul Shungu ambaye aliwahi kuinoa Yanga, amekiri viongozi wa Yanga kumuulizia mshambuliaji huyo ambaye atakuja nchini na kikosi cha As Vita kitakachochuana na Simba Jumamosi
"Yanga wanamtaka Makusu kama ilivyo kwa Simba, lakini nafikiri kutakuwa na kikao tukifika huko Tanzania," Shungu amenukuliwa na Mwanaspoti