Moja ya mambo ambayo Wana Yanga hatupaswi kuyapuuzia ni hili la kuchangia timu ili zipatikane fedha kwa ajili ya kukiimarisha kikosi msimu ujao
Kocha Mwinyi Zahera amejitoa kuisaidia Yanga, amekuja na wazo hili ili fedha hizo zitengeneze kikosi imara kitakacholeta ushindani wa kweli
Kwa sasa Yanga inahitaji kusimama ili iweze kuvutia wawekezaji hapo baadae itakapobadili mfumo wake wa uwendeshaji
Zahera amekuwa muwazi tangu mwanzo wa msimu kuwa mafanikio iliyopata Yanga mpaka sasa hayatokani na ubora wa timu bali ni juhudi binafsi za wachezaji na benchi la Ufundi
Timu inapopata matokeo mabaya itusukume kuchangia zaidi ili msimu ujao tuwe na sababu ya kulaumu na kuwajibishana pale mambo yanapokuwa hayaendi
Kwa sasa wachezaji waendelee kuungwa mkono ili wazidi kujituma lakini lengo kuu liwe kuandaa timu imara kwa ajili ya msimu ujao
Kila shabiki ana shauku ya kuiona Yanga ile ya misimu mitatu iliyopita ambayo mashabiki walikuwa wakienda uwanjani kifua mbele wakiwa na uhakika wa ushindi tu
Kwa sasa hilo halipo, idadi ya mashabiki wanaokwenda uwanjani imepungua kutokana na hofu
Katika kulibadili hili hakuna njia ya mkato hasa wakati huu ambao Yanga inapitia, ni lazima kila mmoja mwenye uchungu na timu awajibike kwa kuchangia ili mambo yaende sawa msimu ujao