Shamrashamra zimezidi kupamba moto ndani ya jiji la Mwanza kuelekea mchezo wa robo fainali kombe la FA kati ya Alliance Fc dhidi ya Yanga
Mashabiki wa Yanga wameipokea timu yao kwa shangwe kubwa hasa ikizingatiwa itaendelea kutumia uwanja wa CCM Kirumba kwa michezo mingine ya ligi
Katika kuonyesha jinsi walivyofurahia ujio wa Yanga, hasa uamuzi wa kutumia CCM Kirumba kama uwanja wao wa nyumbani, mashabiki wa klabu hiyo wa Mwanza na maeneo ya jirani, wameahidi kutowaangusha wenzao.
"Tumefurahi timu yetu kuja kuweka kambi hapa Mwanza, tutaungana wazee wote wa Mwanza kwa kushirikiana na vijana kuona ni kwa namna gani tunaisapoti Yanga yetu iweze kushinda kila mechi, tukianzia na hii ya Jumamosi (dhidi ya Alliance)", Mzee George Shija amenukuliwa na Bingwa
Mwanachama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Chuma wa Nyakato, alisema:
"Wanachama na mashabiki wa Mwanza tunatakiwa kuungana kuiwezesha Yanga kushinda mechi zote zitakazochezwa CCM Kirumba, itakuwa ni aibu kama timu itapoteza mechi ikiwa mikononi mwetu.
"Wenzetu wa Dar es Salaam na mikoa mingine wamefanya kazi kubwa, hivyo sasa ni zamu yetu kuonyesha mapenzi yetu kwa timu yetu ya Yanga."