Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga leo wanashuka kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Alliance Fc katika mchezo wa robo fainali kombe la FA (ASFC)
Kikosi cha Yanga kiliwasili jijini Mwanza tangu juzi, kimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo ambao lazima utoe mshindi wa kutinga nusu fainali
Mkufunzi wa Yanga Mwinyi Zahera amesema vijana wake wako tayari na ana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi
"Tumejiandaa vizuri kupata ushindi mchezo wa kesho (leo). Tunafahamu mchezo hautakuwa rahisi lakini nimewaambia wachezaji wangu wajitume ili tuweze kushinda," alisema Zahera
Ni mchezo ambao utazikutanisha timu hizo kwa mara ya tatu msimu huu.
Yanga na Alliance Fc zimekutana mara mbili kwenye ligi na Yanga kushinda michezo yote
Mshindi wa mchezo huo atatinga nusu fainali ambapo katika hatua hiyo atachuana na Lipuli Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Samora mkoani Iringa
Yanga leo itawakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu Abdallah Shaibu 'Ninja' anayetumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu, Ibrahim Ajib ambaye ni majeruhi, Ramadhani Kabwili aliyetimkia nchini Rwanda na kikosi cha timu ya Taifa U20 na Gadiel Michael aliyekwenda Afrika Kusini kufanya majaribio
Hata hivyo Zahera amesisitiza kikosi chake kiko imara hata bila ya wachezaji hao na amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanja wa CCM Kirumba kuwaunga mkono katika mchezo ambao wamedhamiria kushinda