Juzi wakati akizungumza kwenye Harambee ya kuichangia Yanga 'KUBWA KULIKO', Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe alizungumza mambo mawili makubwa
La kwanza ni suala la ratiba msimu uliomalizika ambalo lilikuwa kilio cha timu karibu zote zilizoshiriki ligi kuu
Dk. Mwakyembe alionekana kukerwa na suala hilo ambapo aliwataka wahusika ambao ni Bodi ya Ligi na TFF kuwa makini katika upangaji wa ratiba msimu ujao
Dk. Mwakyembe alisema ratiba ya msimu uliopita, haikuwa nzuri kwa timu zilizoshiriki ligi hiyo, kwani walikabiliana na wakati mgumu hasa kwa mechi zilizohitaji kusafiri
Aidha baadhi ya timu mfano Simba ilikuwa na mechi za viporo zilizofikia 12
Alisema kutokana na hilo, wizara yake itasimamia kwa ukaribu kuhakikisha ratiba ya msimu ujao inakuwa haina changamoto nyingi
La pili linahusu kutungwa sheria ambayo itadhibiti idadi ya wachezaji wa kigeni ambao wanaruhusiwa katika mchezo mmoja kwenye ligi
Dk Mwakyembe alisema Wizara itazungumza na TFF kuhakikisha wanatengeneza sheria ambayo itaruhusu wachezaji wa kigeni wasiozidi watano kucheza kwenye mchezo mmoja
Msimu uliopita TFF iliongeza idadi ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa kutoka saba mpaka 10 huku ikiruhusu wachezaji wote kutumika kwa pamoja
Dk Mwakyembe alisema ni lazima walinde vipaji vya wachezaji wa ndani hivyo watadhibiti idadi ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kucheza kwenye mchezo mmoja