Beki Abdallah Shaibu 'Ninja' aliyemaliza mkataba Yanga bado anasubiri simu ya viongozi wa timu hiyo ili asaini mkataba mpya
Ninja mmoja wa wachezaji waliotumikia sana Yanga chini ya Mwinyi Zahera msimu uliopita, amesema bado hakuna mazungumzo yaliyofanyika kati yake na Yanga
Hata hivyo amesema mkononi anazo ofa kutoka timu kadhaa zikiwemo za nje ya nchi
"Mkataba wangu umemalizika Yanga na bado sijazungumza na viongozi kuhusu mkataba mpya"
"Hata hivyo nawaambia mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi.. Kama sitacheza Yanga basi nitajiunga na timu kubwa zaidi, " alisema Ninja ambaye hakutaka kutaja jina la timu hiyo akiahidi kubainisha kila kitu baada ya siku chache
Kumekuwa na sintofahamu kuhusu hatma ya Ninja hasa baada ya Yanga kusajiliwa wachezaji wapya wanne wa safu ya ulinzi
cutYanga imewasajili mabeki Lamine Moro, Mustapha Suleyman na Ally Ally huku ikielezwa kuwa imemnasa Ally Mtoni
Mabeki hao wanaungana na Kelvin Yondani na Andrew Vicent ambao bado wana mikataba Yanga
Uongozi wa Yanga umeahidi kukamilisha michakato yote ya usajili mwishoni mwa wiki hii na kuweka hadharani kikosi kwa ajili ya msimu ujao
Yanga inapaswa kukamilisha usajili wa michuano ya CAF Juni 30 kwani tarehe ya mwisho kuwasilisha vikosi kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa ni Julai mosi