Mshambuliaji Amissi Tambwe amemaliza mkataba kunako klabu ya Yanga na uongozi wa timu hiyo umeweka bayana kuwa hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao
Lakini mashabiki wa Yanga wataendelea kumkumbuka Tambwe kwa mafanikio aliyoipa timu hiyo misimu mitano aliyocheza
Tambwe aliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2015/16 na 2016/17 huku akiibuka kuwa mfungaji bora msimu wa 2015/16 akifunga mabao 21
Ndiye mchezaji wa kigeni anayeongoza kwa mabao ligi kuu ya Tanzania Bara akiwa amefunga mabao 73 katika misimu sita aliyocheza Tanzania
Tambwe anashikilia rekodi ya kipekee ya kufunga hat-trik, akiwa amefunga mara sita
Mkali huyo wa mabao kutoka Burundi ataendelea kubaki kwenye vitabu vya kumbukumbu kwenye soka la Tanzania
Baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga, Tambwe alirejea kwao Burundi ambapo amesema licha ya kuondoka Yanga, ataendelea kuikumbuka timu hiyo kwani ni sehemu ambayo amepata mafanikio zaidi
Tambwe alijiunga na Yanga usajili wa dirisha dogo msimu wa 2014/15 baada ya kuachwa na Simba dakika chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa
Inaelezwa usajili wake ulikamilishwa ndani ya ofisi za TFF kuhakikisha mchezaji huyo anaitumikia Yanga