Beki Andrew Vicent Chikupe amesema usajili uliofanywa na Yanga msimu utaifanya timu hiyo iwe moto wa kuotea mbali msimu ujao
Aidha amesema kuimarishwa kwa safu ya ulinzi kutafanya isiwe kazi rahisi kwa timu pinzani kuweza kupata ushindi dhidi ya Yanga
Yanga imesajili walinzi wanne wa kati Lamine Moro, Ally Mtoni, Ally Ally na Mustapha Suleyman ambao wataungana na yeye Chikupe na mkongwe Kelvin Yondani huku hatma ya beki Abdallah Shaibu 'Ninja' ikisubiri uamuzi wa mwisho wa mabosi wa Yanga
Hata hivyo ujio wa walinzi hao unamaanisha kutakuwa na changamoto kubwa ya kupata namba kwenye kikosi cha kwanza
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera hutumia zaidi mifumo ya walinzi wawili wa kati na wawili pembeni
Hata hivyo Chikupe amesema hali hiyo itawafanya wajitume zaidi ili kumshawishi kocha kuweza kuwapa nafasi
"Changamoto itakuwepo hilo kila mmoja mpaka hivi sasa ameshaona, lakini kikubwa ni kufanya mazoezi vizuri na mwalimu ndio ataamua nani acheze kulingana na mahitaji yake,"Chikupe aliliambia Mwanaspoti
"Ukipata nafasi inabidi uitumie vizuri kwelikweli, sasa hapo ndio washambuliaji wa timu pinzani watakapokuwa wanakutana na changamoto nyingine"
Msimu uliopita Yanga ilikuwa na changamoto kubwa kwenye safu ya ulinzi ikiwategemea walinzi watatu tu, Yondani, Chikupe na Ninja
Kutumika mfululizo kwa wachezaji hao kulipelekea kupata majeraha ya mara kwa mara hivyo kuathiri mipango ya timu
Ni Ninja aliyecheza michezo mingi ukilinganisha na wenzie Yondani na Chikupe kwa kuwa hakuwa akipata majeraha ya mara kwa mara