Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' leo inashuka kwenye uwanja wa Taifa kuikabili Harambee Stars katika mchezo wa kwanza wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za michuano ya CHAN inayohusisha wachezaji wa ndani
Mchezo huo unakumbusha 'mtanange' wa mwezi uliopita uliopigwa nchini Misri kwenye michuano ya Afcon na Kenya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 licha ya Tanzania kutangulia mara mbili
Hii itakuwa nafasi kwa Stars kulipa kisasi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa nchini Kenya August 04
Kaimu kocha Mkuu wa Stars Etienne Ndayiragije amesema baada ya kujifua kwa wiki moja, vijana wake wako tayari kwa mchezo huo na wana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi
Watanzania wameaswa kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kuiunga mkono timu yao
Tanzania imekuwa na rekodi ya kufanya vizuri inapocheza mbele ya mashabiki wake, bila shaka rekodi hiyo itaendelea leo