Yanga imeanza ligi vibaya kwa kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru
Matokeo hayo hayakuwafurahisha wengi lakini yabidi kuyakubali kwa kuwa ni sehemu ya matokeo ya mpira wa miguu
Pamoja na kufungwa leo, Yanga ilikosa nafasi nyingi, wachezaji walionyesha juhudi za kutafuta bao la kusawazisha lakini tatizo lilikuwa kwenye umaliziaji
Bado kuna kazi inapaswa kufanyika hasa katika ushambuliaji
David Molinga aliyeanza mchezo wa leo, ameonekana kuwa na 'kitu' mguuni, pengine anahitaji muda zaidi
Balinya, Sibomana na Sadney leo hawakuwa kwenye ubora wao, pengine uchovu umechangia
Ikumbukwe Yanga ilicheza mchezo mgumu sana August 24 nchini Botswana kisha ikasafiri kurejea Tanzania kwa siku mbili ikitua usiku wa kuamkia August 26
Wachezaji wamepumzika siku moja tu kisha kurejea tena dimbani
Hata bao walilofunga Ruvu Shooting, ni kutokana na kukosekana kwa umakini kwa safu ya ulinzi ya Yanga
Bila shaka mchezo huu utalisaidia benchi la ufundi kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kuelekea mchezo dhidi ya ZESCO
Pengine kocha Mwinyi Zahera atalazimika kutafuta michezo ya kirafiki kuendelea kuimarisha timu kabla ya kuivaa ZESCO
Kuna karibu siku 15 za maandalizi kabla ya mchezo huo