Mashabiki wa Yanga mkoani Mwanza wameeleza kutofurahishwa na matokeo ya sare ya bao 1-1 iliyopata Yanga dhidi ya Pamba Fc kwenye mchezo wa kirafiki
Mchezo huo uliopigwa dimba la CCM Kirumba jana, mashabiki hao waliishuhudia timu yao ikiponea chupuchupu na kipigo kutoka kwa Pamba iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani kwa muda mwingi
"Tumekuja uwanjani tukiwa na matumaini tutashinda lakini hali imekuwa tofauti," alisikika shabiki mmoja
"Timu yetu haiko sawa yani naona kama timu ya msimu uliopita ilikuwa kali kuliko hii"
"Mwenendo huu unatukatisha tamaa, yani tunatoka sare na Pamba yenye wachezaji pungufu?"
Aidha baadhi ya mashabiki walimshushia lawama kocha Mwinyi Zahera, huku wengine wakitaka uongozi wa Yanga umuondoe
Baada ya mchezo, Zahera alisema walitengeneza nafasi nyingi lakini walikosa bahati ya kutumbukiza mpira wavuni
Alikiri kuwa washambuliaji wake wanasumbuliwa na hali ya kukosa kujiamini
Amesema ana imani muda utafika watatumia nafasi kufunga mabao
Yanga inaendelea na maandalizi ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya ZESCO United ambapo keshokutwa Jumanne itashuka tena dimbani kucheza na Toto Africans
Mchezo huo utapigwa uwanja wa Nyamagana